17/04/2026
"PROF JAY NI GIANT GORILLA WA BONGO FLAVA
KUTAMBULISHA albamu ya Machozi, Jasho na Damu, ilitoka "Bongo Dar es Salaam", "Jina Langu", halafu "Ndiyo Mzee". Mikwaju mingine iliyofuata ni “Piga Makofi” aliowashirikisha Simple X na Sos B, “Niamini”, aliofanya na familia yake ya HBC, Big W***y na Fanani. “Tathmini” alibatua na Jay Moe, “Nawakilisha”, aliowaalika AY, Black Rhino, Complex na Adili.
Vyuma vingine ni “Na Bado”, “Salamu Bibi na Babu”, “Yataka Moyo” na “Machozi, Jasho na Damu”, uliobeba jina la albamu. Fanya mapitio upya kuanzia mwanzo. Hesabu ni tracks 11. Urefu ni dakika 53. Ukianza kusikiliza, hakuna kupeleka mbele wala kuskip, kila tufe lina-makes sense. Hii ndiyo mantiki huwa hakuna ubishi, Machozi, Jasho na Damu inapotajwa kuwa ni moja ya albamu bora kabisa za Bongo Flava.
Albamu mbili; Funga Kazi 2000, vilevile Machozi, Jasho na Damu, zilitosha kumpa Prof Jay legendary status si tu kwenye jumuiya ya Hip Hop Afrika Mashariki, bali kwa sanaa ya Afrika. Jay ni legend. Jay ni giant gorilla. Vyovyote unavyoweza kumtafsiri, Jay ni monstrous size kwenye utamaduni wa Bongo Flava.
Machozi, Jasho na Damu ilitoka Desemba 2001. Mwaka 2002, yalikuwa majuma 52 ya makusanyo kwa Prof Jay. Show mkoa kwa mkoa, hadi kuvuka mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wakati huohuo ilikuwa miezi 12 ya hekaheka za jikoni, maandalizi ya pishi jipya, Bongo Records, kwa audio engineer, P Funk Majani.
“Priii priii eti promota anabeep, naamua kumpigia bila aibu anajisifu,” ilikuwa salamu ya Prof Jay, jina la wimbo ni “Promota Anabeep”, with Mgosi Mkoloni, michambo mikavu kwa Nyangema Promota aliyevaa suti na kandambili. Anamwahidi msanii paradiso, halafu anampiga kizinga cha nauli na kugongea fegi. “Nyambaaf”, kwa sauti ya Mkoloni. Ndivyo albamu “Mapinduzi Halisi”, ilivyotambulishwa.
Desturi ya Jay ilikuwa kuandika historia katika kila albamu, ndivyo alivyofanya kwenye “Zali la Mentali” ndani ya Mapinduzi Halisi.
Unaweza kuzuia mvua lakini siyo heshima ya Prof Jay kwenye Bongo Flava. Mei Mosi, 2026, Bongo Flava Honors itafanikisha the long overdue induction ceremony ya Jay. 710 Garden, Kawe historia itaandikwa. Sugu The Jongwe atasherehesha tukio.
Ndimi Luqman MALOTO".