Chitanda stories

Chitanda stories Kwa simulizi za kusisimua, kutisha, kuelimisha na kuburudisha kutoka kwa mwandishi KELVIN CHITANDA.

Unaweza pia kufuatilia simulizi za sauti kupitia ukurasa wa YouTube unaoitwa Chitanda stories.

SIMULIZI FUPI: PATASHIKA NAFSINIMWANDISHI: KELVIN CHITANDAMAWASILIANO: 0629387308"Hapana bosi sio k**a nimefeli hapana i...
27/01/2023

SIMULIZI FUPI: PATASHIKA NAFSINI
MWANDISHI: KELVIN CHITANDA
MAWASILIANO: 0629387308

"Hapana bosi sio k**a nimefeli hapana ila."

"Ila nini wewe huna lolote, nilifanya makosa sana kukuamini na laiti ningejua nisingejisumbua"

Mimi ndiye niliyekuwa bosi wake. Nilimkazia macho, sura nikakunja nikauvaa ubosi haswaa. Kwa wakati huo nilijifanya kutopenda longolongo. Chitanda mimi sikuwa Chitanda yule mliyekuwa mmemzoea. Sikuwa Chitanda niliyekuwa nagalagazwa na mpenzi wangu Senorita. Moyo ulinishangaa, nafsi ikanisuta. Kikasalia kicheko tu, kicheko cha chini chini baada ya Beatus kuondoka zake.

Mezani nilisalia mwenyewe. Kikombe cha kahawa mezani. Kiko mdomoni, pembeni yangu kulikuwa na kiti kitupu. Hakikuwa na mtu, ni ambacho alikalia Beatus. Mezani kulikuwa na karatasi nyeupe peeee. Ilikuwa na michoro isiyo na kifani. Ni michoro niliyokuwa naichora mwenyewe nilipokuwa namkaripia Beatus. Yaani nilifanya k**a wafanyavyo waalimu wanapomkaririsha mwanafunzi wafundishapo wanafunzi kadhaa kwenye meza kwa kikoloni inaitwa table teaching.

Nilichukua kikombe kilichokuwa kimetulizana mezani. Muda wote kilitulia tu bila kuchangia chochote katika maongezi yetu mimi na Beatus. Nilikunywa funda la kwanza nikameza, nikanywa funda la pili nikafanikiwa kumeza. Niliazimia kunywa funda la tatu lakini kabla sijafanya hivyo simu yangu iliita.

'Kriiiiii Kriiiiii Kriiiiii Kriiiiiii' iliita kwa kunguruma tu bila kutoa sauti yoyote. Si kwa milio ya simuni wala kwa wimbo wowote wa msanii. Ni kawaida yangu, ndiyo ni kawaida sana kwa simu yangu kutokuwa na mlio. Ni aidha niweke mngurumo ama iite kimya kimya. Sijui ni mazoea ama!

Sikujali kuhusu mlio. Nilipokea kisha nikasogeza simu sikioni.

"Haloo bosi" sauti ilisikika simuni. Jina hilo nilishalizoea hasa katika mazingira ya Dar es salaam. Sio hilo tu bali yapo mengine niliitwa nayo, tajiri, mheshimiwa, kiongozi, papaa, chief, na mengine mengi ya karma hiyo. Hata jina langu la Chitanda lilianza kufifia. Jina ambalo nililipenda sana, nilikuwa na lengo la kulifanya jina hilo kuwa miongoni mwa majina yatakayozungumziwa nchini.

"Naaam naongea na nani?" Niliitika nikaongeza na swali kwa juu.

"Unaongea na Inspekta Odalicus Sixbert, afsa usalama Taifa"

"Mmh kulikoni?"

"Usijali Mr. Chitanda kwa muda mrefu tumefahamu k**a wewe ni jamabazi sugu hapa jijini, jijini Dar es salaaam"

"Mmh jambazi?" Niliuliza kwa mshangao k**a vile nilikiwa sifahamu chochote. Mshangao wangu haukufanya sauti ya simuni kusitisha maongezi. Aliendelea kuongea.

"Eeh ila kwa vile mtandao wako ni mkubwa tumekiri hatukuwezi kwa lolote. Maana mara uonekane hauna hatia mara tushindwe kukuk**ata kabisa, mara tushindwe pa kuanzia. Mimi k**a afsa usalama Taifa nilipenda nikuombe utusaidie kitu"

"Mmh kipi hicho?" Niliuliza swali lingine. Nilikuwa tayari nimeshakubali kuitwa jambazi ingawa sikuwa na wasiwasi wowote. Nilijua mbinu za kutumia endapo k**a zilikuwa mbinu tu za kunitia hatiani. Simu ikiwa bado sikioni nilikumbuka kitu. Nilikumbuka kuhusu mkwara niliokuwa nimempiga Beatus baada ya kumhisi kuvujisha siri. Nilihisi labda alinizunguka na kutoa taarifa katika ngazi za usalama ili kusalimisha nafsi yake. Niliwaza hivyo kwani yeye tu ndiye niliyekuwa nimemdokeza kuhusu tukio la wizi lililokuwa linafuatia.

"Eeh tunaomba uisaidie serikali kuhusu kile kinachoendelea Kibiti!" sauti simuni iliongea hayo ikatulia kusubiri jibu langu.
"Mmh niisaidie serikali? Sasa serikali na mimi nani mwenye nguvu? Au mnataka kuniingiza mtegoni?"

"No...no..no sio hivyo Mr. Chitanda"

"Oh ok endelea, ni kwa namna gani nitaisaidia serikali?"

"Tunataka uwe mpelelezi pale Kibiti kuhusu mauaji yanayoendelea. Tunajua wewe ndiye mtu sahihi utakayekuja na solution ya hili tatizo. Lakini pia utatusaidia kuwafahamu wanaofanya mauaji haya kwasababu wewe una mtandao mkubwa k**a nilivyotangulia kusema hapo awali"

"Sawa, lakini nitawezaje kufanya hivyo?" Niliuliza ingawa sikuwa na hakika k**a angeeleza k**a nilivyokuwa nimemaanisha. Hata hivyo alinielewa swadakta kabisa.

"Usijali kuhusu ulinzi, usijali kuhusu pesa za kuendeshea zoezi. Kuhusu ulinzi utakuwa unashirikiana na jeshi la Kibiti kuanzia jeshi la usalama pamoja na jeshi la polisi. Pesa za uendeshaji utapewa. Lakini pia bila kusahau utataja kiasi utakachokihitaji k**a posho ya zoezi" sauti ilisikika ikatua vema kwenye ngoma ya sikio langu la kushoto. Ilisikika ikakoma kisha kimya kikafuata. Bila shaka niliyekuwa nasubiriwa kusema neno nilikuwa mimi.

Baada ya kufikiri kidogo nilimeza funda la mate nikawa tayari kuongea chochote.
"Inspekta" nilianza kwa kuita.
"Naam bosi" inspekta aliitika akarudia tena kuniita bosi.

"Milioni mia tatu taslimu"

"Hamna shida bosi, naomba kesho Jumatano tukutane nje ya benki ya NMB, Kibiti"

"Benki? Pesa yangu itumwe kwenye akaunti namba yangu masaa manne kabla ya kazi kuanza. Kwahiyo namaanaisha kesho kabla ya saa moja pesa yangu niipate"

“Sawa bosi nipe dakika tano”

“Ok sawa!” nilikubaliana naye nikakata simu.
Ya kwanza, ya pili, ya tatu, ya nne ni dakika hizo. Simu yangu ilikuwa makini sana kuzihesabu. Ilihesabu kwa maringo ya hali ya juu. Moyo nao haukuwa nyuma, uliongeza mapigo ikawa mara mbili yake. Kuna nafsi iliyokuwa inanisuta na kuniambia nisichukulie kawaida.

‘No free lunch in America’ nafsi ilizidi kunisulubu. Moyo nao haukuacha kukoma. Ulizidisha mapigo ikawa kero. Kuna wakati nilitamani nizime simu lakini nikasema hapana ngoja nione itakuwaje yaani ‘liwalo na liwe’.
‘Twiririii’ mngurumo wa kuingia ujumbe simuni mwangu ulisikika. Hapo mapigo ya moyo yalirejea upya, yaliongezeka kasi yake. Haja kubwa ilikuwa inasukuma nguo yangu ya ndani, haja ndogo nayo ilikuwa mbioni kuchomoza.
‘Ila hawa sio k**a wanataka kuniweka mikononi mwao? Serikali ishirikiane na jambazi? —Jambazi sugu. Mimi hii nahisi ni danganya toto tu, nisipoangalia naweza kuozea jela kirahisi sana’ niliwaza huku nikifanya zoezi la kufungua ujumbe uliokuwa umeingia simuni mwangu.

Licha ya kutandwa na wasiwasi pima niliomba ujumbe uliongia uwe wa pesa k**a nilivyokuwa nimefikiri. Nilifanikiwa kufungua ujumbe ukasomeka hivi;

“Ndugu mteja wa NMB Umepokea kiasi cha shilingi 300, 000,000.00 kwenye akaunti yako inayoishia na 5020. Tembelea Benki ya NMB au wakala aliye karibu yako ili uweze kutoa kiasi chochote cha pesa. NMB karibu yako!” ujumbe ukakoma.

‘Mmh ujambazi sasa basi, kupanda daladala basi tena. Nitawamisi niliokuwa nafanya nao kazi k**a akina Beatus—kwa sasa mimi siyo wa karma yao tena. Kwa sasa mimi si’ wakuangalia mpira kwenye vibanda umiza tena, si’ wa kunywa juisi za miwa zilizotengenezwa bila viwango. Hata hivyo naomba tu niwakumbuke wazazi wangu ili nipate baraka zao hata ikifika hatua ya mwenyezi kuwanyakua.’

Niliinuka nilipokuwa nimekaa kisha kwa furaha nikaanza kurukaruka huku nipiga kelele za ushindi. Lo! Nishtuka baada ya kushtuliwa na aliyekuwa ameketi kwa pembeni yangu. Alikuwa mdada aliyekuwa ameupamba vema uso wake. Vishimo vidogo kwenye mashavu yake na macho legelege aliyokuwa nayo viliupamba uso wake.

“Mmh kwani nipo wapi?” niliuliza kwa mshangao mkubwa sana.

“Upo kwenye daladala ya Makumbusho kwani vipi?”

“Ndoto”

“Ndoto? Imefanyeje tena? Maana me nimeambulia kusikia ukisema ‘kupanda daladala sasa basi nikahisi labda kuna lolote umeliona humu garini. Labda kuna aliyeingia na misukule. Imekuaje kaka?” Alinidokeza akanitandika swali bila huruma. Angejua!
“Hapaa usijali nilikuwa ndotoni tu. Lakini ni ndoto ya kawaida tu. Hamna lolote baya”

Nilijihisi aibu sana kwa yale yaliyokuwa yamenitokea mbele ya mrembo ambaye alichukua umakini wake wote kuniuliza kilichonitokea. Sikumsimulia nilichoota nikamwacha abaki na maswali kichwani. Safari iliendelea ingawa sikuwa na hamu ya kulala tena. Mkononi nilishika kitabu cha SAFARI YA MAPITO nilichokuwa nakipeleka kwa mteja aliyekuwa amenielekeza anapopatikana na anuani yake—Makumbusho.

‘Mmh ndoto zingine bwana sijui zina maana gani?’ niliwaza nafsini. Sikuwa na jibu la moja kwa moja ingawa nilikumbuka kilichonifanya nipitiwe na usingizi—Madeni. Madeni yalinizonga kitu ambacho yalikuwa yananifikirisha kila wakati.

‘Kwanini ile ndoto isingekuwa ya kweli tu’ niliongeza kuwaza. Hata hivyo isingewezekana hata kidogo kwani siku zote maji hayapandi mlima. Kwahiyo kuhusu milioni mia tatu zilibaki kuwa za kwenye ndoto tu tena ndoto ya mchana.

MWISHO

PATA NAKALA YA KITABU CHA SAFARI YA MAPITO KWA BEI YA SHILINGI ELFU KUMI TU. MIKOANI TUNATUMA, KWA WALIO DAR UNALETEWA. WASILIANA NASI KWA NAMBARI 0629387308.

Kelvin Chitanda,
Dar es salaam, Tanzania.

SIMULIZI: SITOISAHAU SIKU YA MWAKA MPYAMWANDISHI: KELVIN CHITANDAMAWASILIANO: 0629387308Jina langu ni Derick Machaku. Ba...
20/01/2023

SIMULIZI: SITOISAHAU SIKU YA MWAKA MPYA
MWANDISHI: KELVIN CHITANDA
MAWASILIANO: 0629387308

Jina langu ni Derick Machaku. Baba yangu alifariki kwa ajali mbaya sana ya gari alipokuwa anaelekea kijijini kusalimia. Tangu hapo mimi na mdogo wangu Meshack tulikuwa tumeianza safari ya kuishi na mzazi mmoja tu yaani single parent family. Maisha yetu yalikuwa magumu sana kwasababu mama ndiye aliyekuwa tegemeo letu kwa kila kitu. Yaani kuhusu tule nini tuvae nini ilikuwa ni jukumu la mama bi Janeth Nchakali.

Kwa wakati huo nilikuwa nipo darasa la sita wakati mdogo wangu yeye alikuwa yupo darasa la kwanza. Shule tulisoma kwa taabu sana. Hamna aliyejitolea kumsaidia mama yangu. Ndugu wa baba nao hawakuwa na muda na sisi hata kidogo, kila moja alishika hamsini zake. Baada ya kifo cha baba ndugu zake baba walianzisha vimbwanga kwa mama. Kwanza walichukua kila kitu wakajimilikisha kuanzia shamba la migomba ambalo lilikuwa msaada mkubwa kwetu. Lakini pia walichukua baisikeli iliyokuwa inatusaidia kwa mambo madogo madogo pale nyumbani. Walifanya hivyo kwasababu ndugu wa baba hawakuwa wanampenda mama hata kidogo, walionesha waziwazi kumchukia mama. Walimchukia sana. Walichokuwa wanadai wao ni kwamba mama alikuwa anatokea kwenye familia ya kichawi. Niliumia sana.

Siku zilisonga mbele. Tuliendelea kupokea malezi kutoka kwa mzazi mmoja tu yaani mama. Na k**a ilivyo kuwa mtu atakunyima tonge la ugali lakini sio maneno. Ndivyo ilivyokuwa kwani nilikuwa nadokezewa maneno mengi sana kuhusu bibi yangu mzaa mama. Rafiki zangu walikuwa wananiambia kuwa bibi ni mchawi mkubwa sana. Mwanzo nilichukulia kawaida nikijipa moyo pengine walikuwa na nia ya kutuchonganisha tu mimi na bibi yangu.

Siku zilivyozidi kwenda mbele minong’ono nayo iliongezeka. Bibi yangu alikuwa na tatizo la kusikia lakini walimwengu walichombeza kuwa usiku alikuwa anasikia vizuri tena bila shida yoyote. Kuna muda nilikuwa najiuliza maswali mengi sana, nilikuwa najiuliza wao walijuaje kuwa bibi yangu mchawi? Hata hivyo sikupata majibu sahihi ya maswali yote niliyokuwa najiuliza nikapuuzia.

Shule nilimaliza kwa taabu sana. Hata hivyo mtihani wa kuhitimu darasa la saba nilifanya vibaya nikafeli. Sikuona haja ya kuendelea na masomo katika hali ngumu ya kiuchumi ya familia yetu. Mdogo wangu Meshack aliacha shule akiwa darasa la nne. Sio k**a hakupenda kuendelea la hasha, ni kwasababu alifeli mtihani wa darasa la nne wakati huo hakutaka kurudia darasa. Bila shaka maisha magumu ya familia yetu yalimchosha. Ni kipindi ambacho nilikuwa na umri wa miaka kumi na tisa wakati huo mdogo wangu Meshack alikuwa na umri wa miaka kumi.
****
Siku moja jioni nikiwa nimepumzika ndani nilisikia kelele kwa nje. Ni k**a vile walikuwa hawaelewani katika kile walichokuwa wanaongea. Yaani ni k**a vile walikuwa na sitomfahamu kati yao. Huyu anaongea hili, mwingine anaongea lile. Niliingiwa na hofu sana. Nilichokuwa nawaza mimi ni kwamba labda Meshack alikuwa amemuumiza mtoto huko alipokuwa anacheza. Kupitia dirisha nilichungulia nikaona watoto wengi sana. Baadae watu waliongezeka, watu wazima nao waliongezeka. Nilizidi kuwa na hofu sana moyoni. Mama yeye alikuwepo jikoni kwa ajili ya maandalizi ya chakula cha jioni. Nakumbuka alikuwa anapika wali maharage kwasababu licha ya umaskini wetu tulikuwa tunapenda sana kula wali kila siku ya ijumaa.

“Hodiii, hodi wenyewe hapaa. Wenyewe nyumba hii jamani”

Watu wale waliita kwa msisitizo mkubwa sana. Waliita kwa sauti wakasisitiza kwa vitendo kupitia viganja vyao. Walikuwa wanagonga mlango kwa nguvu sana. Sauti za watu kuita zilimshtua sana mama. Aliacha kupika akatoka nje. Alipotoka nje alipokelewa na umati wa watu waliokuwa wanamtazama kwa huruma sana. Wapo waliokuwa wanalia ingawa wengine walijikaza kisabuni. Wenye moyo wa ukak**avu walimweleza mama kilichotokea ndipo mama alipoanza kuangua kilio. Kilio cha mama kilinifanya nitoke nje ili nami nipate kufahamu kilichokuwa kinaendelea. Nilitoka nje nikauliza.

“Kuna nini jamani? Mbona mmeandamana?” Niliuliza nikiwa na hofu pima.

“Ni mdogo wako Meshack, amefariki. Hatujui kilichomtokea lakini sisi tumemkuta akiwa amefariki. Shingo yake imevunjika, kichwa chake kimepasuka”

Sikuwa na muda wa kuendelea kuuliza maswali tena. Nilisogea mpaka ulipokuwa umelazwa mwili wa mdogo wangu. Nilichuchumaa nikafunua nguo iliyokuwa imemfunika ndipo nilipokutana na mwili wa mdogo wangu Meshack. Mwili mzima ulikuwa umetapakaa damu, kichwa kilikuwa kimepasuka vibaya sana. Niliumia sana kushuhudia mwili wa mdogo wangu akiwa hayuko hai tena, kibaya zaidi chanzo cha kifo hakikujulikana. Kiukweli ulikuwa ni msiba mzito sana ukizingatia kifo cha mdogo wangu kilikuwa cha kutatanisha.

Mama yangu alilia sana jioni ile, alilia mpaka akapoteza fahamu. Fahamu ziliporejea alilia tena, alilia mpaka macho yakakoma. Siku hiyo kifo kilikuwa nimetembelea nyumbani kwetu kikanyakua uhai wa mdogo wangu Meshack. Kifo hakikuwa na huruma kwa mdogo wangu hata siku moja, hakikumhurumia mama aliyekuwa anapoteza fahamu mara kwa mara. Taratibu za mazishi ya mdogo wangu zilifanywa. Majirani walikuwa karibu sana nasi kutufariji kwa maneno murua sana katika kipindi chote tulichokuwa tumeondokewa na mpendwa wetu. Mdogo wangu alizikwa kwenye makaburi ya kanisa Katoliki la kijiji chetu cha Miomboni.

Siku zilizidi kwenda mbele. Kumbukumbu zote kuhusu kifo cha mdogo wangu Meshack zilipotea k**a upepo. Maisha yalizidi kusonga mbele. Hata hivyo watu walizidi kunilisha sumu kuhusu bibi yangu. Baada ya kifo cha mdogo wangu walisema kuwa Meshack alitolewa kafara na bibi. Waliongeza kwa kusema kuwa bibi yangu alikuwa na cheo kikubwa sana kwenye chama chao. Niliendelea kupuuzia maneno yao lakini kumbe lilikuwa ndio kosa langu nambari moja kwasababu sio kwa yale yaliyokuwa yamenitokea siku ya mwaka mpya wa tarehe 01.01.2023.

Siku hiyo ilikuwa ni siku ya mfano wa siku niliyokuwa nimezaliwa. Ni kumbukumbu mbaya sana ambazo kila nikizikumbuka nashindwa kabisa kuyakabili machozi yangu. Zogo lilianza siku moja kabla ya mwaka mpya. Siku hiyo niliota ndoto mbaya sana zilizoninyima usingizi. Ilikuwa mara niote bibi yangu anaolewa na jini, mara niote nimezungukwa na viumbe wa kutisha tena katika msitu mnene mithili ya msitu wa Amazon.

Viumbe hao wa kutisha walikuwa wanatema vitu mfano wa miale ya jua lakini haikuwa inaunguza. Wapo kati yao waliokuwa wanatoa sauti kali sana za kunguruma. Moyo haukutulia kwenye damu. Derick mimi wa ndotoni akili iliniruka nikachanganyikiwa. Sikuwa na namna ya kufanya kwani hata kiroba changu cheusi nilichokuwa nimekipachika kwenye kwapa yangu ya kushoto nilikidondosha. Niliendelea kuchochora tu kuikimbia hatari ile iliyokuwa inanikabili. Hata hivyo ilikuwa mara nikimbie kwa kasi mithili ya umeme, mara niruke kimo kirefu kinyume na uwezo wangu wa kawaida. Nilikuwa mithili ya roboti au k**a vile nilikuwa nimeongezewa nguvu fulani ya ziada. Hata hivyo nilik**atwa kisha watu wa ajabu wakaja na kunifunga nyororo kwenye mikono yangu. Kutokana na mshtuko wa ndoto hiyo ya kutisha niliamka ndoto ikakoma.

Kupitia dirisha nilichungulia ili nijue k**a kulikuwa umepambazuka ama la kwasababu mpaka wakati huo nilikuwa sina simu wala saa ingawa kuhusu elimu ya shule ya msingi nilikuwa nimeshahitimu. Nilipotazama nje nilibaini ilikuwa kati ya saa saba au nane. Ama kwa lugha iliyozoeleka naweza kusema ulikuwa ni usiku wa manane. Niliendelea kulala japo usingizi wa maruerue kutokana na ndoto niliyokuwa nimeota hapo kabla.

Haukupita muda nilisikia sauti ya mtu kulia. Nilisikiliza sauti kwa makini kusikiliza ilikokuwa inatoka sauti nikafanikiwa kubaini. Ni mama yangu ndiye aliyekuwa analia. Alikuwa analia sana, alilia mpaka uvumilivu uliponishinda. Nilitoka chumbani kwangu kwa tahadhari kubwa sana. Mlango wa chumba changu ulistiriwa na kanga tu. Hata kabla sijaufikia mlango wa chumba cha mama yangu nilisikia sauti ya mtu kutembea lakini sikubahatika kumuona. Niliwasha kibatari nikakutana na kitu cha ajabu sana. Damu nyingi sana ilikuwa imetapakaa kutokea kwenye chumba cha mama.

Niliingia mpaka chumbani kwa mama nikakutana na mama akiwa ameshafariki dunia. Mwili wake ulikuwa umeloa damu. Nililia sana siku hiyo. Ni siku ambayo kiukweli. Niliendelea kulia mbele ya mwili wa mama uliokuwa unavuja damu mithili ya maji bombani. Niliacha kulia baada ya kugundua kitu cha ajabu sana kwenye mwili wa mama. Mwili wa mama haukuwa na kichwa. Hata hivyo sikuwa na haja ya kuendelea kulia kwasababu ilikuwa imeshatokea. Niliinuka pale nilipokuwa nalia nikaelekea chumbani kwangu kwasababu bado ulikuwa usiku wa manane. Nilipofika sebuleni nilikutana na kitu kingine cha ajabu sana. Nilikutana na kiumbe kisicho na macho kikiwa kimebeba kichwa cha mama. Umbo la kiumbe hicho lilifanana na binadamu isipokuwa chenyewe hakikuwa na macho. Nilidondoka nikapoteza fahamu pale pale.
***
Asubuhi niliamka nikiwa na uchovu sana. Kila kiungo cha mwili wangu kilifanya kazi kivyake. Mkono wa kulia ulikinzana kiutendaji na mkono wa kushoto. Mkono wa kushoto ulikuwa na unafuu kidogo lakini si kwa mkono wa kulia. Huo sijui niseme ulikuwa umepooza ama ulishika ganzi kutokana labda na kuulalia usiku mzima. Shingo ilikuwa inazunguka kwa tabu, kichwa kilikuwa kizito. Yaani k**a nilikuwa na kiungo kilichokuwa kinafanya kazi yake vizuri labda moyo tu uliokuwa unafanya kazi yake ya kusukuma damu. Nilitoka nje nikamfuata bibi yangu ili nimpe taarifa ya kifo cha mama lakini sikumkuta. Nilienda kwa mzee Gamba nikamjulisha kuhusu kifo cha kutatanisha cha mama.

Niliongozana na mzee Gamba hadi nyumbani kwa ajili ya taratibu za mazishi. Kwa hakika mwaka huo mpya wa mwaka 2023 ulinijia vibaya sana ndio maana sitoweza kuisahau kabisa siku hiyo ya mwaka mpya. Kichwa kiliniuma sana. Kichwa kilinikong'ota kikanishikisha adabu, macho nayo yalinizogoa. Macho yalipoteza uwezo wake wa kutazama vizuri. Yaani k**a ningekuwa mjini ningefanya hima kwenda kumuona daktari.

Watu waliopata taarifa ya kifo cha mama yangu walikuja na kunipa pole. Wapo walionea huruma ingawa wengine hawakujali hata kidogo. Ndugu wa baba wote hawakutokea msibani, sio k**a hawakupata taarifa la hasha. Walipuuzia tu kwa makusudi. Ni kwasababu walishakana kutujua, walisema mama alikuwa anatokea kwenye familia ya kichawi. Sio hilo tu, walifika mbali na kusema kuwa mimi sikuwa damu yao kabisa.

Taratibu za mazishi ya mama zilifanywa na mzee Gamba aliyekuwa ametokea kuwa karibu sana na sisi tangu kifo cha baba mwaka 2019. Mwanzo nilijua pengine ni yeye ndiye aliyekuwa anatufanyia hayo yote kwasababu zake binafsi lakini kumbe nilikuwa nawaza tofauti kabisa. Usilolijua. Fununu zilianza kusambaa mazishini. Minong’ono ilivuma kwa kasi sana, ni kuhusu kifo cha mama yangu.

Watu walivumisha habari kuwa bibi yangu ndiye aliyekuwa amemuua mama yangu. Hawakuishia hapo, waliongeza kusema kuwa bibi alikuwa amemuweka mama kwenye chumba che kufuli chakavu. Ni muda sana hakijafunguliwa. Maneno ya watu yalinitia hasira sana. Ibada ya mazishi ilipofika mwisho nilienda moja kwa moja mpaka nyimbani kwa bibi kwasababu hakuwepo mazishini. Nilipofika nilichomoa upanga niliokuwa nimeuficha nikamjeruhi bibi vibaya mno.

Niliendelea na zoezi mpaka nilipoona amepoteza fahamu. Bibi alidondoka Puuh! Kichwa kilikuwa kinavuja damu mithili ya maji bombani. Nilipoona nimefanya tukio nilitoka ili nirudi msibani lakini ile natoka tu nilipokelewa na vijana watatu waliokuwa wanavuja jasho. Waliponiona na panga lililokuwa linavuja damu waliamini tayari nilikuwa nimeshafanya mauaji. Walinibeba msobemsobe mpka msibani.

Tulipofika nyumbani nilipokelewa na vipigo vya wanaume wenye hasira kali. Baada ya muda mmoja wao alishauri jambo la busara sana. Alishauri kuwapigia Polisi wakafanya hivyo. Hazikupita dakika nyingi gari la Polisi lilifika nyumbani nikachukuliwa. Kesi yangu haikuwa na mizunguko hata kidogo. Nilisomewa kesi nikaswekwa jela kwa kesi ya mauji. Hamna aliyekuwa upande wangu, wote walikana kunijua. Moyoni nilikabiliwa na maumivu yasiyokoma. Moyo haukupata nafuu hata kidogo. Moyo wangu uligubikwa na simanzi tele. Mpaka sasa naendelea kutumikia kifunguo nikisubiri huruma ya mwenyezi Mungu ama msahama wa Rais panapo majaliwa. Ama kwa hakika nitasahau siku zote ila sio siku ile ya mwaka mpya.

Instagram: Chitanda stories
YouTube: Chitanda stories

SIMULIZI FUPI: DUNIA INA MAMBOMWANDISHI: KELVIN CHITANDAMAWASILIANO: 0629387308“Mmh kumbe maisha si lelemama hata kidogo...
02/01/2023

SIMULIZI FUPI: DUNIA INA MAMBO
MWANDISHI: KELVIN CHITANDA
MAWASILIANO: 0629387308

“Mmh kumbe maisha si lelemama hata kidogo”
Nilijisemea huku nikizipiga hatua kuelekea pale alipokuwa amelezwa mama yangu. Mama alikuwa anavuja damu mwili mzima kutokana na kupigwa na kucharazwa mapanga na watu wasiojulikana alipokuwa anatoka sahambani. Haikuwa mara ya kwanza. Ama naweza kusema siyo k**a mama yangu alikuwa wa kwanza kufanyiwa vitendo hivyo vya kikatili la hasaha. Wengine walikuwa wananyongwa, wengine walikuwa wanabakwa ingawa wapo waliokuwa wananafanikiwa kukimbia.

Waliokuwa wanakumbana na madhila hayo wengi walikuwa wanawake na wazee wasiojiweza. Hakukuwa na fununu yoyote kuhusu sababu ya watu hao kufanya vitendo hivyo ingawa serikali iliahidi kufuatilia.
Hata hivyo kabla hata hawajafuatilia balaa zito lilitokea kwa mama yangu. Balaa lililokuwa limeamsha ari mya kwa wanakijiji wa kijiji chetu cha Mkanazawa kuandamana mpaka kwenye serikali ya kijiji.

Siku tatu zilipita pasipo mama yangu kupata matibabu yoyote. Madaktari waligoma kumtibu mama yangu kwa kigezo cha pesa, hatukuwa na pesa kabisa. Sikuwa na uwezo wa kupata kiasi cha pesa kilichokuwa kimesemwa na madaktari. Familia yetu ilikuwa single parent family kwani baba alifariki miaka mingi sana iliyokuwa imepita. Kisa cha kifo chake kilishangaza watu, baba alipotea kwa muda wa siku tatu mfululizo. Jitihada za kumtafuta zilifanyika lakini haikusaidia kitu. Polisi nao walishirikiana na wanakijiji kumtafuta baba yangu lakini bado jibu lilikuwa lile lile, baba hakupatikana.

Zilipita siku saba ndipo masalia ya mwili wa baba yalikutwa porini karibu na bonde la kijiji chetu. Ni masalia tu ndio yaliyokuwa yameonekana. Mabaki ya nguo yaliyokuwa yameloa damu, mabaki ya viungo k**a kichwa viganja vya mikononi na nyayo pamoja na mifupa kadhaa. Vyote hivyo vilishaanza kuoza kutokana na mvua iliyokuwa inaendelea kunyesha. Mama alilia sana, nami nililia mpaka nilipoona inatosha. Hamna aliyekuwa ananijali, kila mmoja alijali hamsini zake tu. Polisi waliruhusu mabaki ya mwili wa baba yazikwe kule kule porini.

Mama alikosa matibabu kabisa. Hamna daktari aliyejali kuhusu mama, kila mmoja alikuwa bize na mambo yake. Siku ya tatu mama alipoteza maisha, nililia sana. Kwa wakati huo nilikuwa na miaka kumi na tano, mdogo wangu Kelvin alikuwa na miaka tisa kwa wakati huo. Tulipokea jina jipya la kuitwa yatima mapema sana.

“Ama kweli maisha si lelemama” nilirudia tena maneno hayo huku chozi likiendelea kunitoka. Nilikabidhiwa mwili wa mama kwani hospitali ya kijiji chetu haikuwa na monchwari kabisa. Nilipata msaada wa gari la hospitali lililokuwa linatumika kwa dharura. Kwa msaada wa gari la hospitali nilifikishiwa mwili wa mama nyumbani.

Hakukuwa na ndugu aliyekuwa upande wangu, ndugu wa baba walikana kunijua kwa wakati huo. Hawakuwa na habari yoyote na mimi. Walichokuwa wanaamini wao ni kwamba mama yangu alimuua baba ili mama aishi kwa uhuru na mambo yake. Sidhani k**a kulikuwa na ukweli juu ya hilo. Kwa upande wa mama yeye walizaliwa wawili tu yeye na kaka yake lakini kaka yake alifungwa miaka mingi iliyopita kwa kesi ya kumpa mimba mwanafunzi.

Alikuwa mwenyekiti wa kijiji cha Mkwizu kijiji jirani na tupokuwa tunaishi sisi. Hata hivyo ni k**a vile alifanyiwa njama tu kutokana na kujali sana maslahi yake na kubania ya wengine.

Taratibu za mazishi zilifanywa na majirani wenye mapenzi mema ambao walikuwa na huruma kwangu. Mzee Jongo ndiye aliyekuwa amefanikisha kila kitu. Mama yangu alizikwa bila fununu yoyote kuhusu waliohusika katika mauaji hayo. Shida ni kwamba kijijini kwetu tulikuwa tunaishi kiujamaa hivyo ilikuwa ngumu sana kuvujisha siri hasa za tukio baya k**a hilo.
****
Baada ya mazishi tuliendelea na maisha ya kawaida mimi na mdogo wangu Kelvin. Maisha yetu yalikuwa magumu sana kwani tulikosa mwelekeo kutokana na kutokuwa na uangalizi ama malezi thabiti. Majirani na wanakijiji kadhaa wenye huruma walikuwa wanantusaidia mahitaji muhimu k**a chakula na mavazi ya shule kwa mdogo’angu Kelvin kwani mimi kutokana na mikikimikiki ya maisha niliacha kabisa shule. Niliacha shule nikiwa kidato cha pili. Hata mtihani wa taifa sikufanya. Sikuona kabisa sababu ya kuendelea kusoma katika maisha magumu kiasi kile. Kila wakati nilikuwa nawalaani waliokuwa wamedhulumu uhai wa mama yangu kipenzi kwasababu mama ni mama tu.

Juma la kwanza lilipita tangu tumzike mama yangu. Fununu zilianza kusambaa, fununu zilizagaa kuwa waliomuua mama wanamsaka mdogo wangu Kelvin kwa udi na uvumba. Sababu ya kumsaka ni kwamba siku mama alipopoteza maisha alikuwa na mdogo wangu Kelvin lakini Kelvin yeye alikimbia baada ya kuwashuhudia wauaji. Wauji waliamini Kelvin aliwafahamu hivyo ingewaletea shida baadaye.

Fununu zilitufikia kwasababu mtu atakunyima chakula lakini sio maneno. Tulichukua tahadhari ili kuwaepuka wauaji wabaya. Nilimzuia Kelvin asiende tena shule kwani nilijua wangemnasa akiwa anaelekea ama akiwa anatoka shule. Seuze alikuwa na tatizo la kutosikia vizuri ndo’ kabisa. Muda wote Kelvin alikuwa anashinda ndani tu. Yaani k**a ingelikuwa kipindi kile cha COVID 19 ungelisema alikuwa anajikinga na Corona.

Usiku tukiwa tumelala tulikuwa tunasikia vishindo ishara ya watu kutembea karibu na nyumba yetu iliyokuwa imejengwa na tofali za kuchoma na kuezekwa na nyasi za kondeni.
Vishindo vya watu kutembea vilikuwa vinanitisha sana. Siku moja kulipokucha nilichukua jukumu la kwenda kutoa taarifa kwenye serikali ya kijiji chetu lakini walionekana kutowajibika katika hilo. Pengine waliogopa kuingilia vita isiyowahusu ama pengine walishalishwa chao.

“Sasa sisi tukusaidie nini?”

“Mnaweza kunisaidia ulinzi kupitia mgambo wa kijiji”

“Ulinzi? Sasa mgambo waache kulinda kijiji wakulinde wewe peke'ako.Ebu acha zako basi!”

Mwenyekiti wa kijiji alionesha kutokuwa tayari kabisa na nilichokuwa nimeomba. Kwanza suala langu hakulichukulia kwa uzito tena.
Siku zilizidi kwenda mbele pasipo kutokea chochote kibaya. Ilifikia hatua tukajisahau na kujisemea kuwa labda yalishapita. Siku moja moja Kelvin alikuwa anaenda shule na kurudi salama. Hamna kilichotishia usalama wake. Pengine ni kwasababu alikuwa anakwenda shule kwa makundi tofauti na awali.

Siku moja usiku wa manane niliona mwanga mkali sana ulikuwa unamulika pale tulipokuwa tumelala. Kelvin alikuwa amelala fofofo, hakufanikiwa kushuhudia kuona mwanga ule uliokuwa unamulika chumbani. Kadri muda ulivyokuwa unasogea mwanga ulikuwa unaongezeka chumbani. Nilipochunguza kwa umakini nilibaini kuwa nyumba yetu ilikuwa inaungua moto.

Nilimwamsha Kelvin kisha kwa tahadhari kubwa sana nikamtoa nje. Niliweka tahadhari pima dhidi ya wauaji waliokuwa wanamsaka Kelvin ili wakamilishe azma yao. Bila shaka walidhamiria kumuua ili wapoteze ushahidi. Nilitoa vitu vya muhimu tukasogea chini ya mti ambao ulikuwepo nje ya nyumba yetu. Tulikaa chini ya mti mpaka asubuhi. Asubuhi kulipokucha nilielekea mpaka kwenye ofisi ya kijiji. Nilienda na mdogo wangu Kelvin kwani nilikuwa nahofia wangemuua.

Tulipofika kwenye ofisi ya kijiji nilisimulia kilichotokea lakini bado uongozi wa kijiji uligoma kunisaidia. Ni k**a vile walikuwa na mioyo migumu ambayo haikuwa tayari kunisaidia. Walifanya k**a vile walikuwa na mkataba wa kuishi milele. Tulilia sana pale kwenye ofisi ya kijiji lakini wapi, tulilia mpaka machozi yakakoma.

Tulirudi mpaka tulipokuwa tumehifadhi vitu vyetu lakini havikuwepo. Mwili wote ulinyong’onyea kwa yale tuliyokuwa tunapitia. Nilihisi pengine kulikuwa na watu waliokuwa wanatufuatilia kwa ukaribu.

“Sasa tutalala wapi?” Kelvin aliuliza kwa uchungu mkubwa sana moyoni.

“Unawaza kuhusu kulala tena, kulala tutalala tu hata kwenye mti fikiria kuhusu kula” Nilimjibu lakini hakuwa anafahamu chochote. Alikuwa anaangaza macho huku na kule bila mafanikio. Sijui alikuwa anatafuta nini lakini kabla hajasema lolote nilimvuta mkono huku nikimsindikiza kwa maneno.

“Twende polisi”
“Polisi?”
“Ndiyo twende tukaripoti”
“Mmh kaka mimi naogopa Polisi”
“Ebu twende bwana. Tusipofanya hivyo tutakufa. Wauaji watatufikia na kutumaliza”

Licha ya kuwa aliogopa Polisi lakini aliogopa zaidi baada ya kumwambia tutauliwa na wauaji waliokuwa wanatusaka. Alikubali kuongozana na mimi tukaelekea mpaka kituoni. Kituo cha Polisi kilikuwa inapatikana kijiji cha jirani yetu kijiji cha Kwizu. Ili kufika kijiji cha Mkwizu ilikuwa ni lazima uvuke mto na kwa kuwa kilikuwa kipindi cha masika mto Mkwizu ulikuwa umejaa maji.

Tulipoufikia mto Kelvin alionesha kuwa na woga zaidi. Kiukweli Kelvin alikuwa anaogopa sana maji hasa maji mengi yanayokimbia. Hata hivyo nilimnyanyua nikambeba mgongoni kisha kwa tahadhari pima nikaingia ndani ya maji. Chini nilikanyaga takataka, na vipande vya miti vilivyokuwa vimeoza kutokana na kukaa kwenye maji muda mrefu. Maji yenye kasi yalikuwa yanajitahidi kunivuta lakini tulifanikiwa kuvuka.

Upande wa pili wa mto tulipokelewa na vipigo vikali. Fahamu zetu zilirejea hospitali tukiwa tunaendelea kupokea matibabu. Pembeni kulikuwa na Polisi aliyekuwa amejitambulisha kwetu k**a afande Marco Dotto. Pembeni yake kulikuwa na nesi wa k**e ambaye nililitambua jina lake k**a nesi Zai.

Nikiwa bado naendelea kusikiliza maelezo ya nesi Zai kuhusu mazingira ambayo tulikuwa nayo mimi na mdogo wangu pale tulipokutwa na wasamaria wema aliingia daktari mmoja ambaye mwili wake ulionekana kuridhika pesa. Alikuwa amenawiri sana. Baada ya kuingia alimtazama yule Polisi kisha akamwongelesha.

“Afande”
“Naam dokta”
“Hawa ni wanao?”
“Hapana, mimi nipo hapa k**a chombo cha usalama. Nimekuja kufuatilia maendeleo yao”
“Oh sawa. Watoto wanaendelea vizuri. Nitawaandikia dawa kisha utaondoka nao”
“Sawa”

Walikubaliana ikawa kweli. Baada ya kupatiwa karatasi yenye dawa tulijongea taratibu mpaka lilipokuwa gari la afande Marco tukaingia garini. Mwendo wa dakika kumi na tano za gari ulitufikisha nyumbani kwa afande Marco. Nyumba ilikuwa ya kawaida tu, haikutofautiana na za wanakijiji wengine isipokuwa nyumba ya afande Marco ilikuwa imejengwa na wakoloni miaka ya sabini.

Tulishuka akatuelekeza ndani tukaingia. Nyumba haikuwa imefungwa, sikushangaa kwani nilijua lazima afande Marco alikuwa na mke wake. Hata hivyo siku moja ilipita pasipo kumuona mke wa afande Marco. Siku ya pili nayo vilevile, hakukuwa na mabadiliko yoyote.
Chakula tulipikiwa na msichana ambaye bila shaka alikuwepo pale kumsaidia kazi afande. Nilimfahamu kwa lugha ya mtaani k**a beki tatu. Jina lake halisi lilkuwa Halima.

Kadri muda ulivyokuwa unazidi kusonga mbele ndivyo tulivyokuwa tunazidi kuzoeana. Afande Marco alituchukulia k**a wanae. Hivyo Halima tulimchukulia k**a dada yetu wa kufa na kuzikana. Halima alikuwa mweusi ingawa weusi wake haukuwa wa kuchosha kumtazama. Alikuwa na macho madogo na mashavu ya wastani.

Afande Marco alikuwa bize sana na kazi yake. Bila shaka kazi ya upolisi sio lelemama hata kidogo. Fikiria apambane kuhusu unyanyasaji wa watoto, unyanyasaji wa kijinsia ama apambane na wanaouza na kutumia madawa ya kulevya, tafrani mtindo mmoja.

Maisha nyumbani kwa afande Marco yalikuwa ya furaha sana. Ilikuwa ni k**a vile tulikuwa tumepata wa kulifuta chozi letu. Huzuni ilianza kutanda ghafla mara baada ya afya ya afande Marco kuingia dosari. Afande Marco alikuwa anakabiliwa na homa za mara kwa mara. Afya yake ilikuwa dhoofu, mwili ulimkongoroka akawa mithili ya kijana mwenye umri wa miaka kumi na tisa. K**a ingekuwa kipindi kile cha COVID 19 wangemteka wakifikiri labda amejizolea Virusi vya Corona.

Afande aliugua mpaka mwili ukakoma. Alitumia dawa zikaisha, alihudhuria hospitali bila mafanikio yoyote. Alitembelea hospitali kubwa zote lakini haikusaidia kitu. Alikuwa ameshanaswa na ugonjwa. Alikuwa wakufa leo wa kufa kesho!

K**a muujiza, afya ya afande Marco ilikaa sawa. Aliendelea na kazi akaungana na askari Polisi wengine katika kulinda raia wa kijiji cha Mkwizu na vijiji vingine vya jirani.

Hazikupita siku tatu, tulipokea taarifa za kifo cha afande Marco. Afande Marco alipigwa risasi na watu wenye hasira kali sana. Taarifa za chinichini zilieleza kuwa afande Marco alikuwa anafuatilia kwa chinichini kuhusu waliokuwa wamefanya mauji ya mama yangu lakini hakufanikiwa. Bila shaka wauaji walikuwa wamejipanga. Wauaji walikuwa na mtandao mkubwa sana. Hivyo afande Marco alipojitanguliza kufuatilia kesi ya mama aliambulia shaba aliyokuwa amepigwa alipokuwa anarudi nyumbani.

Nililia sana niliposikia chanzo cha kifo cha afande Marco. Kwanza nilimchukulia k**a baba yangu, lakini pia kitendo chake cha kukubali kufa kisa kesi ya mama yangu kiliniaminisha kuwa yeye ndiye aliyekuwa msaada kwangu.

Taratibu zote za mazishi zilifanywa na kituo cha Polisi Mkwizu kwa kushirikiana na serikali ngazi ya kata na wilaya. Mke na mtoto wa afande Marco walipoteza maisha katika ajali ya meli ya MV Spice. Tangu hapo afande Marco hakuoa wala kupata mtoto mwingine tena.
Kwahiyo baada ya kifo chake nyumba ya kota tuliyokuwa tunaishi ilichukuliwa na uongozi wa Polisi. Hapo ndipo nilipobaini kuwa Halima hakuwa mwanae, bali alimchukua katika kituo cha kulelea watoto yatima umri wake wa kukaa kituoni ulipokwisha yaani miaka kumi na nane. Halima hakuwa na ndugu wala jamaa, kiufupi hakukuwa na taarifa zozote kuhusu ndugu zake ndipo afande Marco alipomchukua na kuishi nae.

Mimi na mdogo wangu Kelvin tulichukuliwa na dokta Mafuvu. Dokta Mafuvu alihudhuria mazishi ya afande Marco lakini pia ni yeye ndiye aliyekuwa ameupima mwili wa afande Marco kabla ya Polisi kuruhusu mwili kuzikwa. Dokta Mafuvu alikuwa na ukaribu sana na afande Marco, hivyo hakuona shida kutuchukua tukaishi kwake. Mkuu wa kituo cha Polisi Mkwizu aliahidi kufanya uchunguzi kuwanasa wauaji.

Dokta hakuwa na uwezo wa kutuchukua wote watatu yaani mimi mdogo angu Kelvin pamoja na Halima. Hata hivyo Halima alichukuliwa na mkuu wa kituo cha Mwizu. Kwa dokta tuliishi kwa amani. Hamna kibaya kilichotutokea. Mama yaani mke wa dokta Mafuvu aliishi na sisi bila kinyongo chochote, alitupenda, alifurahi kuwa na sisi kiasi kwamba tulijihisi tuko nyumbani kwa baba na mama mzazi. Kelvin alianzishwa shule ingawa umri wake ulikuwa umeenda. Mimi nilipelekwa kusomea kompyuta kozi ya miezi sita. Kwasasa nimefungua steshenari inayonisaidia pesa kichele kwa ajili yangu na mdogo wangu Kelvin. Namshukuru sana yule daktari, Mungu ambariki.

Kadri siku zinavyozidi kusonga mbele nafikiria kufungua banda kwa ajili ya kuuza mikanda ya filamu na kuuza sidii. Wote waliofanya mauaji ya mama pamoja na afande Marco walik**atwa na kuswekwa sero. Kila siku nafanya maombi kwa ajili ya baba yangu, mama yangu pamoja na afande Marco walale mahali pepa peponi. Lakini pia nafanya maombi kwa ajili ya kijiji changu cha Mkanazawa.

WEKA ODA KUPATA NAKALA YA KITABU CHA MWANDISHI ALPHONCE EVARISTER KUPITIA NAMBARI 0719458115.
Alphonce Evarister

UNAWEZA KUPATA SIMULIZI ZA SAUTI ZA MWANDISHI KELVIN CHITANDA KUPITIA UKURASA WAKE WA YOUTUBE UNAOITWA SIMULIZI ZA CHITANDA AMA KUPITIA WHATSAP NAMBA YA 0629387308.

Address

Kibaha
0629387308

Telephone

+255629387308

Website

Alerts

Be the first to know and let us send you an email when Chitanda stories posts news and promotions. Your email address will not be used for any other purpose, and you can unsubscribe at any time.

Contact The Establishment

Send a message to Chitanda stories:

Share