29/07/2026
TUSALI SALA YA ASUBUHI.
+Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Amina.
Ee Baba yetu Mungu mkuu,
Umenilinda usiku huu,
Nakushukuru kwa moyo,
Ee Baba, Mwana na Roho.
Nilinde tena siku hii,
Niache dhambi, nikutii.
Naomba sana Baba wee,
Baraka yako nipokee.
Bikira safi, ee Maria
Nisipotee nisimamie,
Mlinzi mkuu malaika wee.
Kwa Mungu wetu niombee
Nitake nitende mema tu,
Na mwisho nije kwako juu. Amina.
NIA NJEMA.
Kumheshimu Mungu wangu
Namtolea roho yangu,
Nifanye kazi nipumzike
Amri zake tu nishike.
Wazo, neno, tendo lote
Namtolea Mungu pote
Roho, mwili, chote changu,
Pendo na uzima wangu
Mungu wangu nitampenda,
Wala dhambi sitatenda.
Jina lako nasifia,
Utakalo hutimia.
Kwa utii navumilia
Teso na matata pia.
Nipe, Bwana, neema zako
Niongeze sifa zako. Amina.
•SALA YA MATOLEO.
Ee Yesu, kwa mikono ya Bikira Maria, na kwa maungano na sadaka yako kuu, ninakutolea sala, matendo, masumbuko na furaha zangu zote za leo. Ee Yesu, ufalme wako utufikie. Amina.
BABA YETU.
Baba yetu uliye mbinguni, jina lako litukuzwe. Ufalme wako ufike. Utakalo lifanyike duniani k**a mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku. Utusamehe makosa yetu, k**a tunavyowasamehe na sisi waliotukosea. Usitutie katika kishawishi, lakini utuopoe maovuni. Amina.
SALAMU MARIA.
Salamu, Maria, umejaa neema; Bwana yu nawe, umebarikiwa kuliko wanawake wote, na Yesu, mzao wa tumbo lako, amebarikiwa.
Maria mtakatifu, Mama wa Mungu, utuombee sisi wakosefu, sasa na saa ya kufa kwetu.
Amina.