05/07/2025
BURKINA FASO YAFUTA LESENI ZA MASHIRIKA YA MISAADA YA KIGENI, YASITISHA MASHIRIKA YA KIRAIA: HATUA MPYA YA UDHIBITI WA SERIKALI YA KIJESHI.
Serikali ya kijeshi ya Burkina Faso imechukua hatua kali kwa kufuta leseni za mashirika manne ya misaada ya kigeni na kusimamisha shughuli za mashirika mawili ya kiraia, kwa mujibu wa hati za Serikali zilizoonwa na shirika la habari la AFP.
Katika amri zilizotiwa saini katikati ya Juni, Serikali ilieleza kuwa mashirika hayo yamevunja masharti ya kisheria yanayotakiwa kwa uendeshaji wa Taasisi zisizo za kiserikali Nchini humo. Mashirika mawili ya kigeni yamesimamishwa kwa muda wa miezi mitatu, ambapo moja linadaiwa kuvunja sheria za usalama wa data.
Tangu mapinduzi ya Septemba 2022 yaliyoingiza madarakani utawala wa kijeshi chini ya Kapteni Ibrahim TraorΓ©, Burkina Faso imejikita katika kampeni ya kurejesha kile inachokiita "uhuru wa kitaifa". Serikali imeongeza udhibiti dhidi ya mashirika ya kiraia, Wanahabari, na Taasisi za kimataifa, ikidai kuwa hatua hizi ni za "kulinda usalama wa Taifa" dhidi ya mashambulizi ya makundi ya itikadi kali.
Katika miezi ya hivi karibuni, Serikali ya kijeshi ya Burkina Faso imeendesha ukandamizaji dhidi ya vyombo vya habari vya kimataifa. Mnamo Aprili 2024, mamlaka zilisitisha matangazo ya BBC Africa na Voice of America kwa kipindi cha wiki mbili, zikidai kuwa vyombo hivyo viliripoti taarifa zisizo na ushahidi kuhusu jeshi la Burkina Faso kuhusika na mauaji ya Raia.
Mataifa ya magharibi yamekuwa yakishtumu hatua hizi k**a ukandamizaji dhidi ya uhuru wa kujieleza na kushiriki katika masuala ya kijamii. Afisa wa kidiplomasia wamefukuzwa Nchini kwa madai ya kushiriki shughuli za "kuvuruga utawala".
Hatua hizi mpya za serikali ya kijeshi ya Burkina Faso zinaashiria kuendelea kwa sera za udhibiti dhidi ya mashirika ya misaada na vyombo vya habari, katika jitihada za kudhibiti taarifa na shughuli za kiraia Nchini humo. Wakati huo huo, Nchi inaendelea kukabiliwa na changamoto kubwa za usalama kutokana na mashambulizi ya Makundi ya itikadi kali.
ZAWI MEDIA