15/09/2022
N G A B U J I
(27).
Ahadi ni deni na msema kweli ni mpenzi wa Mungu. Ilikuwa jioni ikawa asubuhi. Asubuhi asubuhi Bwana Mwarabu alitinga anaendesha teregita nina maana trekta lisilo na majembe yake.
Walisalimiana na baba na pia sisi sote nyumbani.
Hakutaka kupoteza muda, alishusha sanduku la chuma kutoka juu ya trekta na aliliweka chini karibu na ile gari ya baba iliyoko juu ya mawe.
Mara alianza kulishughulikia lile gari, ilimchukua karibu masaa matatu anahangaika, ndipo alipo mwambia baba ikiwezekana apate watu wawili watatu, wamsaidie kuliwasha gari kwa kulisukuma.
Alifanikiwa kuwapata watu na vile vile gari lilipo sukumwa liliwaka. Bwana Mwarabu alizunguka zunguka nalo maeneo ya uwanja wa gurio la zao la pamba, mara kwa mara alitoka na kuingia kwenye gari, anajua mwenyewe alicho kuwa anakifanya. Hakuchukua muda alirudi na aliliegesha gari pembeni kisha alitoka na kukaa pembeni mwa
Hilo gari.
Alitokea mama yangu
akawakaribisha kahawa. Wote wawili walijuimuika pamoja. Walikunywa kwa furaha na kwa vicheko. Baadae alimwambia baba kuwa umefika muda sasa waondoke kurudi Nyambiti. Hivyo trekta ataliendesha baba na gari ataiendeha Bwana Mwarabu. Hivyo Bwana Mwarabu alikusanya vifaa vyake na kisha waliondoka kuelekea Nyambiti.
Siku hiyo baba hakurudi, na kesho yake hakurudi. Siku ya tatu baba alirudi, alitumia pikipiki. Ikawa ndiyo ni kanuni kwake, jioni anarudi nyumbani na asubuhi anaenda Nyambiti kwa kubadirisha usafiri. Leo pikipiki, kesho gari, kesho kutwa anakuwa trekta nakadhalika.
Hali hiyo ilidumu takribani miezi mitatu, baadae tulipata habari kuwa baba amesafiri na Bwana Mwarabu. Wamekwenda Nairobi. Kufanya nini? Sisi hatukuwa na jibu ama majibu. Ujue kuwa haya yote yalitokea bado nikiwa darasa la tatu katika shule ya Shushi. Nini kiliendelea?
Itaendelea.....(28).