23/08/2025
Ushairi Ni Kazi ya Moyo, Fikra na Taaluma.
Na Mkuluwanyika.
Ushairi wa Kiswahili si kazi rahisi na ya kawaida wala si jambo linalotendeka papo kwa papo. Kuunda shairi la Kiswahili lenye mvuto na ubora ni mchakato mrefu unaohitaji utaalamu, hekima na ubunifu wa hali ya juu. Si kazi ya hatua moja tu, bali ni safari ndefu ya ubunifu inayoanzia ndani ya nafsi ya mshairi.
Mchakato wa Ubunifu wa Ushairi
Kutunga shairi awali huanzia na hatua ya kutafuta wazo. Wazo litakaloibuliwa na mshairi laweza kuwa dogo na la kawaida, lakini humlazimu mshairi alichunguze kwa kina, alipime na alichimbue haswaa hadi apate kiini chake chenye utoshelevu wa hakika isiyo na punje ya shaka ndani yake.
Hatua inayofuatia huwa ni kuchagua muundo wa shairi; je, mshairi atatumia aina gani ya shairi? Hapa ndipo mshairi anapoanza kujikuta kwenye changamoto kubwa ya kuzingatia sheria na kaida za ushairi wa Kiswahili. Hizi ni pamoja na uwepo wa vina, mizani , beti na mishororo . Hapa ndipo ugumu unapoanzia kwani inamlazimu mshairi afikirie namna ya kuupanga ujumbe wake ili ufikishwe kikamilifu huku akizingatia sheria zinazoendana na muundo husika,sheria ambazo kwa namna yoyote ile zinahitaji ufundi wa hali ya juu kuzitimiza.
Mshairi huwa hanabudi kuzitambua kaida za miundo ya mashairi ,ili iwe rahisi kuchagua muundo unaoendana na aina ya wazo alilonalo,mfano ikiwa ana wazo la kuandika shairi la wasifu itamlazimu atambue kanuni na taratibu za kuandika utenzi na itakuwa hivyo kwa aina nyingine yoyote ya muundo atakaoutumia ikiwa ni tarbia, ngonjera, ukawafi, kikwamba, zingo, kisarambe na miundo mingineyo. Ulazima huo ni k**a ule wa fundi mwashi anapokabidhiwa ramani ya jengo na eneo la kujenga, humpasa kufahamu je ramani hiyo alonayo yaendana na eneo husika na je jengo atakalojenga litakuwa katika taswira iliyokusudiwa na inayohitajika?
Jambo la Tatu: Mtindo wa Shairi
Mtindo wa shairi unahusu jinsi mshairi anavyowasilisha wazo au ujumbe wake. Hapa kunajumuisha uchaguzi wa maneno, matumizi ya tamathali za semi, na jinsi lugha inavyotumiwa kuunda hisia fulani. Kwa kuwa USHAIRI ni sanaa inayozingatia arudhi nasi lugh ya nathari,mshairi bora anahitaji matumizi umbuji zaidi wa kufahamu lugha na usahihi wa matumizi ya lugha katika shairi. Katika mtindo mshairi anatakiwa kuwa mbunifu na kuhusisha matumizi ya:
* Tanakali za Sauti: Mbinu ya kutumia maneno yanayoiga sauti au hali fulani, au namna kitendo kilivyofanyika.
* Tashbihi: Mbinu ya lugha inayolinganisha vitu au hali mbili tofauti kwa kutumia maneno ya kulinganisha, k**a 'k**a', 'mithili ya', 'sawa na', au 'ja'.
* Istiara/Sitiari: Mbinu ya kulinganisha vitu viwili moja kwa moja bila kutumia viunganishi.
* Jazanda: Kitu au mtu huwakilishwa na kitu kingine kinachofanana naye kwa sifa au tabia. Tofauti na tashbihi, jazanda haitumii maneno ya kulinganisha. Mfano: "Yule mama ni simba."
* Taashira: Matumizi ya lugha ya ishara kuwakilisha ujumbe fulani. Jina au kitu fulani kinatumika kumaanisha kitu kingine chenye uhusiano na kile kilichotumiwa.
* Taswira: Matumizi ya lugha/maneno yanayojenga picha ya hali au jambo fulani kwa msomaji.
* Tashihisi: Mbinu ya kupatia kitu kisicho na uhai sifa za kiumbe mwenye uhai (sifa za kibinadamu). Huu huitwa uhuishaji.
* Chuku: Kutumia maneno yaliyotiliwa chumvi ili kusisitiza ujumbe fulani au kusifia kitu.
* Takriri: Mbinu ya kurudiarudia neno moja au kifungu cha maneno ili kusisitiza ujumbe fulani.
* Tanakuzi: Mbinu ya kusisitiza ujumbe kwa kuambatanisha maneno ya kinyume au yanayokinzana.
* Majazi: Ni ufundi wa lugha ambapo mshairi hutumia majina, majina ya mahali, au majina ya vitu vyenye maana ya ndani au siri.
* Lakabu: Mbinu ya mhusika kupewa au kubandikwa jina na wahusika wengine, ama yeye mwenyewe.
* Semi: Fungu la maneno linapotumika kutoa maana nyingine, badala ya ile ya maneno yaliyotumika. Semi hutumika kuficha ukali wa maneno au kupamba lugha. Kuna aina mbili za semi:
* Nahau: Huwa na vitenzi.
* Misemo: Haina vitenzi.
* Methali: Ni misemo ya hekima yenye maana iliyofumbwa.
* Maswali ya Balagha: Ni maswali yanayoulizwa kutumia tamathali za semi, methali, nahau na hata vitendawili ili kuongeza ladha na undani wa shairi.
Kwakuwa kazi ya mshairi ni kujenga picha katika akili za wasikilizaji na wasomaji, na hili linawezekana tu kupitia matumizi ya hayo mambo yaliyotajwa.
Utoshelezi na Muwala
Safari ya mshairi haiishii katika muundo na mtindo pekee. Ili kulifanya shairi lake liwe bora,mshairi atahitajia utoshelezi na muwala ili ujumbe wake uwe mzito na wenye maana ya kina.
* Utoshelezi: Katika shairi la Kiswahili, maana yake ni hali ya kila ubeti kujitosheleza kwa habari au ujumbe unaompa msomaji ili afahamu maelezo ya ubeti huo kikamilifu. Hii inaendelea kwa mtiririko unaoeleweka kutoka ubeti mmoja hadi mwingine.
* Muwala: Ni mtiririko wa fani na mawazo ulio na mantiki katika shairi. Katika taaluma ya ushairi, kuna aina mbili za muwala:
* Mawazo ya ubeti yanapaswa kufuatana kwa ufasaha kutoka fatahi, mroto, mleo, na kituo ili kuyajenga mawazo kikamilifu.
* Sheria ya pili ni muwala wa beti lazima uwe na mtiririko mzuri wa mawazo kutoka ubeti hadi ubeti. Katika aina hii, mawazo huwa yamefungamana na maudhui ya tungo na huwa yamekamilika.
Hapa, unapochambua kwa kina, utaona ugumu wa utunzi wa shairi. Sio jambo jepesi kwa mshairi kuhakikisha anakamilisha hali ya utoshelezi katika kila ubeti, yaani aeleze jambo lenye maana, lakini wakati huo huo maana hiyo isigongane na maana ya beti nyingine na ilete mtiririko unaoeleweka katika muktadha wa maudhui mama. Mfano, ubeti wa utangulizi wa shairi hauwezi kuwa katikati ya utungo na ubeti wa kaditama hautakiwi kuwa katika mukadima.
Sio Kila Mwandishi ni Mshairi
Kwa ugumu na ukweli kwamba ushairi si kitu rahisi, ndipo ikawa si kila mwandishi ni mshairi.
Waswahili wanasema, "Mashairi bora si ya mtu wa kawaida." Kwa hakika, si kila mtu anaweza kuwa mshairi. Inahitaji hekima na utambuzi wa lugha ya hali ya juu. Washairi ni watu wachache waliopatiwa karama ya kuunda maneno ambayo thamani yake ni kubwa sana. Huenda ndiyo maana kuna usemi usemao, "Ukiondoa vitabu vitukufu vya dini ambavyo vinaweza kuongoa imani, matendo na fikra za watu, vinavyofuata ni vitabu vya ushairi."
Ikiwa mtu anaweza kuyafinya maneno machache kwa mipaka ya sheria na kanuni na yakaleta maana pana, basi ni hakika hawezi kushindwa kuelezea mambo kwa kutumia maneno marefu pasipo kubanwa na sheria ngumu mahsusi. Ndipo ikawa mtu anayeweza kuandika shairi anaweza kuandika kitu chochote nje ya ushairi kwa ufasaha na ubora wa hali ya juu. Ni washairi pekee ambao hutumia taaluma yao ya lugha kufinyanga maneno na kuunda kazi za sanaa ambazo hufikia hisia za binadamu kwa namna ya kipekee,huo ndio msingi wa ithibati ya kuwa kila mshairi ni mwandishi, lakini si kila mwandishi anaweza kuwa mshairi kwa ubora wa kishairi.
Tuuthamini na Kuulinda Ushairi Wetu
Tusiuache ushairi wetu wa Kiswahili upotee. Tusiudharau ushairi wala kuwadharau washairi. Ni jukumu letu kuulinda, kuuthamini, na kuutukuza, kwani ni hazina ya fikra na chemchemi ya lugha yetu. Tutambue mashairi yanatukumbusha kuhusu historia yetu, utamaduni wetu, na maadili yetu. Tuwathamini washairi kwa kutambua athari na mchango wao katika jamii. Ama kwa hakika washairi huacha alama isiyofutika katika historia ya lugha yetu.
Binafsi, sitoyasahau matukio matatu ambayo nayahesabu k**a alama zisizofutika katika sanaa yangu ya ushairi.
Tukio la Kwanza: Niliwahi kuombwa kutunga shairi kuhusu madrasa iliyokuwa katika mazingira magumu. Wanafunzi walisoma barazani, tena katika nyumba ya udongo, na mwalimu wao alitembea umbali mrefu kufundisha bila mshahara wala posho. Nilipoomba kuwasemea, nilitunga shairi na kupaza sauti. Kwa hakika, sauti ilifika mbali na hatimaye madrasa hiyo, kutoka Msambweni, Kenya, imejengwa ya kisasa na mwalimu naye amejengewa sehemu ya kuishi.
Jambo la Pili: Kupitia kero hiyo, nilipaza sauti kuwasemea walimu wa madrasa na hatimaye kukazaliwa UMATA (Umoja wa Maimamu Tanzania). Kupitia umoja huo, semina na makongamano yalifanyika kuendeleza maendeleo ya walimu wa madrasa kiuchumi na kielimu. UMATA ikawa sababu ya taratibu nyingine zenye mlengo wa kutatua kero za walimu wa madrasa kupatikana.
Na Jambo la Tatu: Ni pale nilipochoshwa na kero ya maji iliyokuwa imetamalaki wilayani Ubungo, Dar es Salaam. Nilitunga shairi lenye kuisemea kero hiyo, na shairi likafika hadi kwa wahusika. Hatimaye, kero hiyo ilitatuliwa, na nilishuhudia hilo.
Hivyo, ushairi si fani ya malumbano na majigambo pekee; ni fani yenye kuibua kero na matatizo ya jamii. Ni fani yenye kuunganisha watu na kulinda tamaduni, ni urithi na silaha dhidi ya upotovu wote.
Si mimi tu niliyewahi kuleta athari chanya zenye kunufaisha watu kupitia ushairi. Ni washairi wengi waliopita, waliopo, na wajao, na itabaki hivyo hadi mwisho wa dunia.
Hivyo basi, ushairi uenziwe, ushairi utukuzwe.