19/05/2023
TUWE WALEZI SIO WATESI.
Watoto kwetu baraka, nawala sio laana,
Hawafai kuteseka, au hata kuwakana,
Kile wanacho kitaka, tukizingatie sana,
Tuweni kwao walezi, wala tusiwe watesi.
Kisha tusiwabague, misingi ya kijinsia,
Tena yapaswa tujue, si vyema kuwachukia,
Wakike tuwatambue, na wa kiume sawia,
Tuweni kwao walezi, wala tusiwe watesi.
Tuache kupendelea, tuwapeni haki sawa,
Tukome kuwaonea, nawala kutowagawa,
Hivyo nikuwakosea, majonzi hadi kujawa,
Tuweni kwao walezi, wala tusiwe watesi.
Wote tuwape upendo, tena uwe ni wa dhati,
Tofauti ziwe kando, mbele yao hatuteti,
Yawe mazuri matendo, Kisha kwa kila wakati,
Tuweni kwao walezi, wala tusiwe watesi.