Mwandishi Said Kaita

Mwandishi Said Kaita Ukurasa maalumu wa hadithi kutoka kwa mwandishi Said Kaita. Hadithi zenye mafunzo, kuburudisha na kusisimua. KARIBU.

Afrika yangu!Sehemu pekee ambapo mtu anauamini utamaduni wa majirani kuliko wake
06/01/2026

Afrika yangu!
Sehemu pekee ambapo mtu anauamini utamaduni wa majirani kuliko wake

MWANDISHI: SAID KAITA HADITHI: SARA NAMBA: +255783372139 E-MAIL: saidikaita7@gmail.com MAALUM KWA WATOTO Sara ni mtoto m...
29/05/2022

MWANDISHI: SAID KAITA
HADITHI: SARA
NAMBA: +255783372139
E-MAIL: [email protected]
MAALUM KWA WATOTO

Sara ni mtoto mwenye miaka mitano. Anampenda sana mama yake, hupenda kukaa nyumbani na kujishughulisha na michezo mbalimbali k**a vile kupika kwa kutumia matope. Ambapo, huchota maji, kisha hutafuta mahali ambapo pana mchanga mzuri na kujipikilisha mwenyewe. Ila, michezo yote hiyo hupenda kufanyia nyumbani kwao tu. Huwa hapendi kabisa kwenda kucheza kwa majirani, kwani huhofia sana mama yake akirejea asijemgombeza. Pia, huogopa kupigwa na wenzake kwa kuwa yeye ni mpole sana. Aonapo amechoka hutafuta sehemu nzuri na kutandika kwa vipande vya kanga ambavyo mama yake amempatia k**a vya kuchezea. Michezo hiyo hufanya baada ya kumaliza shughuli zake ndogo ndogo ambazo mama yake humuachia pale nyumbani k**a vile kufagia uwanja wao, kuosha vyombo k**a vile sahani, bakuli na vijiko. Kabla mama yake hajatoka huwa amemwandalia vizuri vitu vyote hivyo na kumuacha sasa yeye apange muda wake wa kuviosha vyombo hivyo. Ifikapo muda wa kula huchukua jiko la mafuta ya taa na kuwasha kwa kiberiti ambacho mama yake alimuonesha atakitumia. Mara nyingi mchana hula wali, kwa hiyo humpasa Sara achukue wali ule na kwenda kuupasha kwa makini kisha hula. Mama wa Sara hupenda kurudi mapema sana baada ya mishughuliko yake ya siku. Siku moja mama Sara alichelewa sana kurudi. Sara alijiuliza sana maswali mengi. Kwa kuwa haikuwa kawaida ya mama kuchelewa hivyo. Kwa vile anampenda sana mama yake, Sara aliijiwa na mawazo ya kwenda kumtafuta mama yake popote alipo. “Lazima nimfuate mama alipo”. Sara alijisemesha mwenyewe kwa sauti ambayo ilionesha ina kiu ya kumuona Mama. Basi kwa ujasiri wake, alivaa koti lake vizuri ambalo aliwekewa na mama wake sehemu ya jikoni. Pindi asikiapo baridi ndipo huvaa. Baada ya kuvaa koti lile na kuhakikisha viatu alivyovaa kamwe havitamuumiza katika safari yake, ilibidi aanze safari. Hakutaka hata kwenda kuwaambia majirani zake huko anakoenda. Alianza safari polepole huku akifuata njia ambayo mama yake huitumia kila siku wakati anarejea kutoka mishughulikoni. Kwa muda huo tayari ilikuwa imeshatimia saa moja kasoro jioni. Tayari jua lilikuwa limeshalala na kuacha sasa anga ikiwa imenuna kwelikweli k**a imepigwa na jua. Alitembea k**a dakika kumi na tano lakini hakupata kukutana na mtu yeyote huko njiani. Jambo hili lilimshangaza hadi kujiuliza. “Leo kuna nini?” Ila, kutokuwa kwa watu vile hakukuweza kumkatisha tamaa. Bali aliendelea na safari hadi alipofika sehemu ambayo ina eneo kubwa sana la mchanga. Sehemu hiyo ilikuwa na kelele ambazo zilileta utofauti kidogo. Alipozidi kukikacha kichanga kilichopo katika eneo lile alishangaa tu kitu kimepita, “Mvuu” Ni sauti tu ya kitu alisikia k**a kimepita japo hakuona chochote. Hakujali chochote juu ya hali iliyokuwa ikitokea. Alianza kuzunguka kuanzia sokoni ambapo mama yake ndipo hufanya kazi huko za upishi. Hapo hakuweza kumkuta, marafiki wa na mama Sara nao walikuwa wameshaondoka muda mrefu sana. Kwa hiyo, hakupata hata mtu wa kumuuliza. Baada ya pale kushindikana alienda hadi bwawani ambapo mama yake huenda kuchukua samaki huko lakini hakufanikisha kuona sura ya mama yake kabisa. Moyo ulimuuma sana kila anapoenda anamkosa mama yake. Ndipo alipoona bora aende katika duka la mchele ambapo mama yake hununua mchele wa jumla. Hapo nako alikuta pamefungwa kabisa. Sura yake ilimjaa huzuni sana. Alijua kabisa mama yake kuna jambo limemsibu, si bure kabisa. Ilibidi arejee nyumbani tu, alipokuwa akirejea nyumban alikutana na jirani yake aitwaye Roja alikuwa na baiskeli. Ilibidi Roja ampatie lifti Sara. Roja alimuuliza maswali Sara "Mbona upo pekee yako? Ulikuwa wapi?" lakini Sara muda wote huo alikuwa amekaa kimya k**a maji ya mtungini yakitafakari nani anakuja kuyanywa Roja alijua kabisa Sara hataki kuongea. Roja alikanyaga pedeli hadi kufikia nyumbani kwa akina Sara. Walipofika hapo walimkuta mama Sara amesharudi na alikuwa ameshaanza kufikiri namna ya kwenda kumtafuta Sara. Sara alifurahi sana kumuona mama yake, pia mama Sara naye alifurahi sana.
Mwisho

FACEBOOK: Saidi Kaita
Twitter:

JINA LA HADITHI FUPI: MSAMAHA WA KWELI ?MWANDISHI: SAID KAITAFACEBOOK PAGE: Saidikaitastories.comBLOG: Saidikaitastories...
12/09/2020

JINA LA HADITHI FUPI: MSAMAHA WA KWELI ?

MWANDISHI: SAID KAITA

FACEBOOK PAGE: Saidikaitastories.com

BLOG: Saidikaitastories.blogspot.com

MAWASILIANO: 0783372139

E-MAIL: [email protected]

Usilolijua ni sawa na usiku wa giza nene. Ni msemo ambao mara chache hutumika katika ndimi za watu ila huwatokea tu muda ambao jambo husika limeshatendeka pia kuwa na uhakika nalo.
Usiku ulioambatana na sauti za mbu zililizunguka eneo alilokuwa amelala Ahata. Sauti zilizojawa hasira kila mmoja wao akiwa anatafuta kitoweo. Kwa ukali wa sauti zile ulisikika k**a mtu akiwa anapiga kinanda kwa utaalamu na hakuna ambaye angeweza kulala kwa sauti zile. Sauti ya makofi ilikuwa ikisikika kila mahali “Paaa... Paaa” kila mtu alikuwa akijihami asing'atwe. Ahata alikuwa amelala chini ya kalavati akiwa amejifunika na mfuko wa kubebea uchafu. Mbalamwezi iliyokuwa iking'aa angani kwa namna yake iliweza kutoa nuru na kufanya watu wengi waliokuwa wamelala pale kushukuru. Muda huo hakuna aliyekuwa akifanya mazungumzo na mwenzake bali kila mtu alifikiria ni nini alichofanya mchana. Upande wa pili wa kalavati nako palionekana vijana wakiwa wamelala kwa kupanga msitari. Aliyepata box la kulalia alishukuru Mungu na aliyekosa basi ilimbidi avumilie. Sauti ya Ahata ilisikika ikwia imejawa na malalamiko juu ya mbu wanavyowasumbua. “Laaaa laaa laaa... hawa mbu ndiyo wameniamlia hivi?... k**a nina ugomvi nao? Eee Mungu embu saidia hawa viumbe wako unaowaona hapa. Tunapata tabu sana katika maisha yetu, nini kabisa tumekukosea? Mchana tunafanya kazi ngumu na hela ndogo, usiku tunalala sehemu ambayo si rafiki kiafya Kabisa. Lini utatutoa huku? Kila siku maombi yangu nimekuwa nikikuomba niondokane na hali hii mimi na rafiki zangu. Ni mwaka wa nne huu umepita tangu nimeanza kuhangaika na haya maisha. Mbona mimi bado tu kiumri lakini maisha yangu yameshaanza kuonekana magumu k**a vile mwamba? Wazazi wangu kufariki ikawa ndiyo chanzo cha mimi kuwa hapa? Ama kweli mwanadamu hata awe ndugu yako vipi muangalie usoni tu sababu moyoni humjui. Kuwa nao makini sana... Leo mimi ni wa kuhangaika hivi kweli? Kwangu mvua ikija sawa naipokea, ikija baridi kali kwangu naipokea na hata ukija upepo mkali vyote vyangu tu. Vyote vinanipiga mimi na wenzangu huku ambao hatuna hata pakukimbilia. Ukikimbilia kibarazani kwa mtu ndiyo hivyo utaitwa mwizi, wanadamu walivyo na roho za kinyama utaona watakavyokufanyia. Eeee Mungu waweke wazazi wangu mahala pema, wambie wameniacha katika hali mbaya sana, ila sina namna ntahesabu nyota weee hadi usingizi unijie”. Mahali hapo palikuwa pamejaa harufu za sigara na bangi. Mipishano ya kukohoa haikuepukika kutokana tu na kazi ngumu za mchana walizokuwa wakifanya nyingine zikiwa ni za vumbi zaidi. Hata k**a ni za vumbi hakuna aliyekuwa na ratiba ya kununua maziwa ili kujiweka vizuri. Ilifikia kipindi Ahata usiku anakula mkate na maji tu.
Alfajiri na mapema ilipowadia sauti za kuwaamsha waislamu kwenda kufanya ibada zilisikika. “swalaaa swalaaa... Swala ni bora kuliko usingizi...” Japokuwa sauti zile zilikuwa ni za kuwajulisha watu kwenda kusali lakini kwa Ahata na rafiki zake ilikuwa ndiyo muda wao kujiandaa na kwenda stendi kubeba mizigo ya abiria. Aliyekuwa na mkokoteni aliufuata na kuuchukua kuanza nao kazi, aliyekuwa na guta naye alifanya hivyo hivyo. Ila kuna baadhi ambao hawakuwa navyo hivyo wao walikuwa ni kubeba mzigo begani tu. Ahata alijiandaa kwa kujifuta matongotongo bila hata kupiga mswaki safari ikaanza.
Palipozidi kupambazuka kila mtu alizidi kuumiza kichwa ni wapi pakupatia kibarua. Hata jua lilipowaka Ahata wala hakujali sababu hata aseme apumzike alijua kabisa mjini hakuna hela ya bure. Ukisema ukaibe dakika utajikuta kwenye tairi. Ahata alionekana akiwa amekaa pekee yake huku akiwa ameshikilia kimfuko cha maji akipunguza kiu. Akiendelea kunywa alitokea jemba lenye miraba minne na kumwambia. “Leta maji hayo”. Ahata alikataa na kutaka kuondoka sehemu ile lakini pande lile la mtu dakika tu alimpiga teke la makalioni, kwa uzito wa teke lile Ahata alianguka chini na maji yakadondoka yakawa hayana hata sura ya kunywewa. Alichafuka kwa vumbi lililokuwa pale chini. Ahata alikuwa ni mdogo sana kwahiyo hata hakuweza kumfanya lolote bali alibaki kulia tu akiwa pale chini jemba lile nalo likawa limeondoka. “Jamaa hili jinga kweli badala litumie nguvu zake kutafuta pesa halali linabaki kuonea watu tu” Ahata alisema, aliinuka na kujikung'uta nguo zake ambazo zilionekana ni chafu sana zimejaa oil tu. “Daa sema afadhali halijachukua vidala vyangu vilivyokuwa mfukoni”. Wenzake walibaki kumwangilia tu sababu hawakuwa na uwezo hata wa kumpiga mwanaume yule.
Usiku ulipoingia kila mtu alianza kuangalia ni wapi atakapolaza mbavu zake na kuanza kuota ndoto za kujenga angani angali amelala chini. Ahata akiwa na rafiki yake walikuwa wakilonga za maisha huyu akinena hivi na yule vile. “Sasa Ahata haya maisha tutaenda nayo hadi lini? Sababu naona kila kukicha hela zenyewe ndiyo hivyo shida tu”. Rafiki wa Ahata alikuwa akinena hivyo kisha Ahata akasema. “Yaani rafiki yangu kwa hali hii mafanikio ni vigumu kwetu. Sababu angalia kwanza hela tunayopata ilivyo ndogo, kazi tunazofanya ni ngumu sana ambazo zinazidi kutuletea maumivu kwenye miili yetu tu. Wala hatutumii hata dawa, nini tunajitakia? Yaani leo mimi nina miaka kumi na mbili lakini sura yangu inaonekana k**a nina miaka arobaini” “Sasa Ahata unaonaje ili tuondokane na hii hali?” Alikaa kimya kwa sekunde chache huku akiwa amempiga mbu aliyekuwa akimng'ata kisha akasema “Mimi hata sielewi”. “Ahata unajua kuna story naambiwaga kuhusiana na hawa watu waliotajirika sana. Wengi unaambiwa walikuwa hoehae k**a sisi tu, mwishowe wakaamua kwenda kujiunga na freemason ndiyo maana wakafanikiwa hivyo. Usiwaone tu wanaendesha magari ya bei ghali hivyo”. Ahata akamuuliza swali. “Freemason ndiyo kitu gani hicho?”. “Ahaa huko unaambiwa ukiingia kuna masharti wanakupa tu ukishatekeleza tu tayari unaanza kufanikiwa” Ahata aliuliza. “Masharti k**a yapi?” “Wengi huwa wanasema unatakiwa umuue mama yako kwa vile ndiye unayempenda sana”. Suala la kumuua mama lilimuuma sana Ahata kwa kuwa anajua uchungu wa mzazi, isitoshe mama yake aliuliwa kikatili sana. “Daaa unajua rafiki yangu hadi hapo mimi siwezi kabisa kusikiliza hilo wazo lako. Kwa sababu kumuua mama wakati mama yangu aliuliwa kikatili na ninajua uchungu wa mzazi weee? Embu hiyo mada kwangu usiiweke kabisa. Yaani nikija kukua na nikijua ambaye aliwaua wazazi wangu kikatili vile yaani atakiona cha mtemakuni”. Rafiki yake alimuomba msamaha Ahata kwa kuwa alimkumbusha maumivu makali ambayo yalimtokea miaka minne iliyopita. Kukatika kwa mazungumzo yale yaliwafanya kila mtu aanze kunyemelewa na usingizi na kulala fofofo. Ikiwa ni usiku wa manani ghafla ilikuja mvua kali dakika chache tu mawingu yalitanda. Mvua ilianza kwa kasi sana na kufanya watu waliokuwa wamelala hapo kulowana sana. Ambao walikwa wamelala chini ya makalavati kilichowashtua ilikuwa ni mafuriko yaliyokuwa yakija kwa kasi sana yakiwa na kila aina ya uchafu, walifanya haraka haraka na kila mtu akaanza kujiokoa na kutoka nje.
******************************************
Ilipopita miaka saba mbeleni Ahata alipata nafasi ya ufadhili kutoka katika shirika la kizungu lililokuwa na makao makuu yake huko Denmark. Shirika lilijukana k**a Youth Talent Arise Organization (Y.T.A.O) ambalo liliweka pia tawi katika taifa la Zatan. Lilishughulika na kuinua vipaji kwa vijana. Ahata alipata nafasi huko baada ya kuonekana kuwa alikuwa na vipaji vingi tu k**a vile uimbaji, uandishi wa hadithi na uchoraji. Siku ya mashindano Ahata alifanya vizuri na ndipo akawa amesajiliwa Y.T.A.O kwa jina la Ahata Esbern. Ambapo Esbern lilikuwa ni jina la mwanzilishi na mmiliki wa Y.T.A.O. Alimpenda sana Ahata na kumhakikishia kuwa atamhudumia vizuri, mmiliki yule alimjengea kasiri ili kumfanya Ahata aishi kwa raha msitarehe. Esbern aliamua kumtembeza Ahata katika mataifa mbalimbali na watu wakamjua zaidi kupitia kipaji chake. Ahata alizidi kukosha nyoyo za watu hadi ilifika kwa mwaka alitumbuiza katika matamasha makubwa zaidi ya mia. Kwa mwaka mmoja tu alipata tunzo nyingi sana. Hadi wizara ya michezo nchini Zatan ilimpatia tunzo kwa namna alivyokuwa akiipeperusha bendera ya Zatan kupitia kipaji chake, kila mtu alimjua Ahata na kuzidi kumpenda, sura yake ilinawiri sana k**a nyota yake ilivyo. Hata na kupata umaarufu vile Ahata hakuwasahau watu wa chini ambao alihangaika nao huko mtaani zaidi ya miaka k**a kumi. Aliwapatia fedha na kufanya Ahata azidi kuimarika kwa rafiki zake. Ndugu wa Ahata ambao walimdhulumu mali za baba yake na kumfukuzia mbali walianza kumtafuta na kutaka wapatiwe msaada, kwasababu mali zile wala hawakuzifanyia maendeleo yoyote. K**a ilivyo pesa za dhuluma siku zote hazinawirishi chochote.
Baba wa Ahata alikuwa ni tajiri mkubwa tu katika eneo alilokuwa amezaliwa. Alikuwa ni tajiri kijana mwenye upendo sana kwa wananchi wenzake. Ahata alipofikia umri wa kujielewa ndipo baba yake akaamua kugombea ubunge. Harata ambaye ni baba wa Ahata alikuwa na wafuasi wengi sana. Lakini mpinzani wake hakuwa na wafuasi wengi japokuwa aligombea kupitia chama tawala cha Zatan kilichojulikana kwa M.K. Mbunge yule kutoka M.K hakupenda hali ile na kuona atashindwa ndipo alipoamua kufanya njama za kumuua Harata, mkewe pamoja na Ahata. Lakini hakufanikisha kumuua Ahata kwasababu siku ya mipangilio yote hiyo Ahata hakuwa nyumbani. Baba wa Ahata na mama walichinjwa kisha vichwa vikazikwa na miili yao kukutwa imetupwa barabarani. Kiongozi wa M.K alipoulizwa na vyombo vya habari alikana katu katu kuwa hakuhusika na mauaji hayo ya kikatili.
Mwenyekiti wa Y.T.A.O nchini Zatan alikuwa akiitwa Simba ambaye alifanikiwa kuwa na watoto wawili, mtoto wake wa kwanza ni wa kiume na wa pili ni wa k**e. Mwanaye wa k**e alijaaliwa uzuri sana hata angeamua kuwania umiss basi angeshinda. Alitumia uzuri wake na kumshawishi Ahata kuwa mpenzi wake. Ahata wala hakusita na kuona kuwa ameamka kitandani na kukuta kifungua kinywa kimeshaandaliwa. Dada huyo alijulikana kwa jina la Aisha. Aisha alijaaliwa uzuri ambao kila aliyemuona mahali fulani basi alisimama na kumuangalia hata dakika moja kabisa. Asubuhi na mapema kwenye vichwa vya magazeti palijaa taarifa iliyokuwa ni habari picha ukisema. “Ahata apata kigori”. Esbern alimpa Ahata hongera sana kwa kuwa amefikia maamuzi mazuri kwa muda muafaka.
Dunia nzima ilisikia na kuona uhusiano huo k**a walivyotambua vipaji vyake. Maandalizi ya harusi yalianza vizuri sana, kadi za mwaliko zilitumwa katika kila kona za dunia. Maandalizi yote yaliwezakufikia mahala pazuri hadi kufika asilimia tisini na tano. Mungu si Athumani dunia haina siri asubuhi na mapema magazeti yalijawa na taarifa isemayo kuwa Ukweli Wabainika kuhusu mauaji ya Harata UK 04. Kichwa cha habari kile kiliwavutia sana wanunuzi wa magazeti na kufanya wanunue wengi sana. Ahata pia alipenda sana kusoma magazeti asubuhi kabla hajaanza maandalizi ya ratiba za siku. Akiwa kwenye bustani amekaa kwa pembeni palikuwa na chai iliyokuwa imewekwa kwenye meza ndogo hivi. Alishtushwa sana na taarifa ile ndipo akaamua kufunua moja kwa moja ukurasa husika. Alianza kusoma gazeti lile ambapo mwisho wa habari ile palionekana picha ya aliyekuwa mbunge wa M.K na sasa ni Mwenyekiti wa Y.T.A.O bwana Simba. Habari ile ilitoa ukweli wote juu ya mauaji ya Harata. Ahata alichanganyikiwa sana baada ya kuisoma habari ile. Aliwasiliana na Aisha awasili nyumbani kwake haraka sana. Aisha hadi anafika pale nyumbani hakuwa anajua lolote kwa kuwa Aisha hakuwa mfuatiliaji wa magazeti sana. Hali aliyomkuta nayo Ahata ilibidi ashangae sana, kisha akamwambia Aisha. “Soma hilo gazeti ukurasa wa nne alafu utaniambia”. “Alilisoma kwa ufasaha na alipokutana na jina la Baba yake pamoja na picha za Baba yake alichanganyikiwa sana. Alianza kujitetea sana kuwa ile habari si ya kweli huku akimuomba wasije wakaachana”. “Ahata ndiyo unataka kuniacha kwa kuwa umejua ukweli wote huo. Ila mimi sikuwa najua kabisaa. Naona ni uongo huo. Wanataka kumchafua Baba tu”. Muda wote Aisha alikuwa akiongea Ahata alikaa kimya tu. Ghafla simu ya Aisha iliita na alipoangalia ni Baba yake ndiye aliyempigia na Ahata akasema.
“Pokea simu yako”.
“uko wapi mwanangu. Nakuomba njoo nyumbani haraka”.
“Baba Niko kwa Ahata hapa”.
Simba kusikia hivyo hapo hapo aliachia simu akaanguka chini na kuzimia. Haraka haraka matabibu waliitwa ili kumshughulikia. Ahata alimjulisha Esbern mkanda mzima na bahati kipindi hicho Esbern alikuwa Zatan ndipo Esbern akamwambia Ahata wakafanye mazungumzo kwa Simba. Ahata na Aisha walielekea moja kwa moja hadi kwa Simba. Muda si mrefu Esbern aliwasili na kumkuta Simba ameshazinduka, Simba alipungua sana mwili kwa taarifa zile. Walimsubiri Simba apate nafuu ndipo wakaanza mazungumzo ya mapatano.
Ilibidi Esbern aongoze kikao bila hata kuegemea upande wowote ule. Bali aliendesha kikao kile kwa lengo la kuwasuluhisha. Palikuwepo Esbern, Ahata, Simba, Aisha na mke wa Simba. “Aaaaa... Ahata najua ni namna gani una hasira, ni namna gani kichwa kinakuuma, ni namna gani unavyofikiria kuwa katika hili unaweza kumkosa Aisha au laa. Pia, unafikiria ni namna gani utakavyopoteza watu muhimu sana ambao wamekutoa katika umaskini na leo wewe ni nyota wa Zatan na hata nje ya Zatan wanakutambua kuwa wewe ni nyota mkubwa mwenye kipaji kweli. Ulitamani sana leo hii uwe unatumia mali zako na familia yako yaani Baba na mama. Lakini kamwe inashindikana na yote hii ni kutokana na namna mtu fulani alivyokufanyia familia yako. Ila Ahata niseme tu kwamba leo hii umejua ukweli wa kifo cha wazazi wako na unataka kulipiza kisasi. Sawa utalipiza kisasi ila jua k**a chuki yenu kamwe haitoisha. Leo ukikubali Simba auliwe tambua hii nayo ni familia hivyo lazima nawo wataanza kupanga namna tu ya kukuua, sababu nawo wanampenda baba yao, wanampenda mama yao na wote wanapendana. Huoni ukifanya hivyo hizi familia zitakuwa ni za kumwaga damu kila kizazi? Kumbuka k**a umezaliwa Mungu ndiye aliyepanga uzaliwe, siku zote yeye ndiye hupanga mtu azaliwe kwa namna atakavyo na mtu akishazaliwa kifo kwake ni lazima. Basi k**a Mungu ndiye muumba wetu yeye ndiye anayeamua ni namna gani vifo vyetu vinavyotakiwa kuwa. Mimi siyo mwamini sana na mambo ya kidini ila napenda kusoma vitabu vya kidini ambavyo vinanipa maarifa sana. Ahata nakuomba legeza moyo wako, shusha hasira yako juu ya hili, angalia suala hili lisije likakuchafulia jina lako kabisa”. Ahata alikuwa amekaa kwa makini akiwa anamsikiliza Esbern ushauri wake. Maneno yale yalimwingia sana na kuyatafakari kwa kina sana. Mazungumzo yalienda vizuri ndipo Ahata akapatiwa nafasi ya kuzungumza yake kutoka moyoni. “Sina mengi ya kunena bali machache ya kupatanishana, siku zote mtu ukiwa na hasira unaweza ukatoa maamuzi ambayo yanawezakuwa ni mabaya sana kwako. Natambua fika kuanza kwa vita humaanisha kumalizika kwa vita na ndipo mgogoro utaisha. Ila niseme tu hili limeshatokea na lilitokea kwa wazazi wangu tena nikiwa mtoto tu. Mimi kulipa kisasi suala hili kwangu ingekuwa ngumu hata k**a Aisha asingekuwa mchumba wangu. Ila yote hii pia ni kwa ushauri mzuri wa Esbern wenye ushawishi na sina hata kukulipa mkuu. Natambua uchungu wa wazazi wangu na namna walivyouliwa kikatili. Sidhani mimi kulipa kisasi ndiyo itakuwa mwisho wa visa hivi, bali ndipo itakuwa mwendelezo wa visa vingine kwa vizazi vya ukoo wa leo na vizazi vya ukoo wa kesho. Nikilipiza kizazi na kizazi kijacho kitalipa hili kwangu. Niseme tu Baba nimekusamehe. Unawezakujiuliza huu ni Msamaha wa kweli?” Simba alijibu harakaharaka, “Ndi... Ndi... Ndiyo ... Lazima niulize Ahata... Huu Msamaha wa Kweli? Sababu najua ni kosa kubwa nililolifanya. Nilifanya mauaji yale kwasababu tu nilikuwa na tamaa na nafasi ile ya uongozi. Uchu wa madaraka ulinifanya niusahau utu kabisa angali na mimi ni mtu. Nilitanguliza matamanio yangu kwa kuwaaminisha wananchi kuwa mimi ni Kiongozi mwema angali sikuwa hivyo. Wengi tunatamani matamanio yetu yakamilike hata kwa kumuangamiza mtu fulani ambaye anaonekana ni k**a kizuizi cha mipango yake”, Ahata alimkatisha Simba maongezi na kusema “Niseme tu kuwa Simba huu ni msamaha wa Kweli”. Simba alishukuru sana na huku Esbern akiwa amemuonesha Ahata kinasa sauti k**a ushahidi wa walichokiongea. Kwa ujumla Esbern alijaaliwa sana maongezi ya ushawishi na ndiyo maana hata aliweza kumshawishi Ahata kutupilia mbali chuki hiyo.
Ahata, Esbern na Aisha baada ya kumaliza yote pale walitoka nje ya geti la Simba kuelekea mahali walipo yaacha magari yao. Hapo nje walikutana na umati wa waandishi wa habari ukiwasubiri kwa hamu sana. Kila mwandishi tayari alikuwa amejikoki maswali ya haraka haraka kwao. Walishangaa sana kukutana na umati wa waandishi wa habari ukiwa wanawasubiri pale nje.
“Ahata vipi ndiyo mipangilio ya arusi imevunjika?” mwandishi aliuliza
“Hatuelewi Ahata asubuhi yote kwa adui yako! Ahata mbona bado uko na Aisha?” wengine wakionekana kudaia. Ni baadhi ya maswali yaliyosikika yakiulizwa na waandishi wa habari. Muda wote Ahata, Esbern na Aisha bado walikuwa wamepigwa bumbuwazi kwa waandishi wa habari waliokuwa wamejaa pale. Ahata alijifikiria kwa sekunde chache alitamani kuondoka lakini alifikiria kuwa kukimbia tatizo siyo kusuhisha tatizo. Alijikaza kiume na Esbern akampa moyo.
“Habarini ndugu waandishi wa habari. Kumradhi nitazungumza nanyi kwa ujumla juu ya yaliyotokea. Maswali machache niliyoyasikia kutoka kwenu bado yapo kichwani nimeyanasa vizuri. Niseme tu kwamba ndugu waandishi wa habari ninyi nawajua vizuri. Lengo lenu kuu ni kupata habari na habari hizo tena ziwe endelevu. Ni kazi yenu na ni jukumu lenu na hapo nitawapa hongera. Natumai mnatamani sana niwapatie majibu ambayo ninyi mnayategemea na siyo yangu. Nipende kusema tu kuwa yote na yote yaliyotokea hayo ni juu yangu na mimi ndiyo muumivu wa yaliyotokea bali kwa jamii ni mfaidishi kwao. Tayari tumeshafanya mazungumzo na Simba na yote yameshaisha na mwafaka tulofikia si kuendeleza vita bali ni kusimamisha vita. Japokuwa siku zote katika chuki za kivita kuisha kwa vita, hivyo lazima kwanza watu wapigane ndiyo vita itaisha. Lakini kwa mimi nimeona kuwa sina Muda wa kuendeleza vita sababu yote hiyo ilikuwa ni mipangilio ya mungu tu. Kulipiza kisasi itamaanisha kuwa na mimi nitakuwa hatarini daima. Sitaki kufanya kuwa hiki kizazi kiwe kizazi cha kumwaga damu k**a Simba alivyokuwa ameanzisha. Maombelezo ya vifo vya wazazi wangu nilishanfanya miaka mingi iliyopita. Wakati huo nilikuwa na mawazo hayo hayo ya kulipiza kisasi. Lakini siku hazifanani kamwe na kila kimbunga kina urefu wake na nguvu yake. Natambua kuwa dunia itashangaa kwa maamuzi yangu ila ndiyo hivyo jukumu huitwa hukumu kwasababu ya maamuzi tu. Kuhusu uhusiano mimi na Simba bado uko karibu. Bado ninamheshimu akiwa k**a mwenyekiti wa Y.T.A.O na baba mkwe wangu mtarajiwa. Kusema hivyo ninamaanisha kuwa maandalizi ya arusi yapo palepale na tarehe iko palepale. Ninashukuru kwa gazeti lililochapisha habari hiyo, kwasababu limeweza kunijulisha mambo makubwa ambayo sikuwa nayajua. Nitajitahidi kufanya nao mazungumzo kwa jambo hili. Hivyo, sina budi kusema kuwa kumradhi kwa mliyokuwa mkiyategemea. Nikushukuruni kwa ujaji wenu hapo”. Ahata na Aisha waliingia kwenye gari moja na Esbern akawa amepanda kwenye gari lake. Madereva walirudishia vioo na Safari kuanza. Aisha na Ahata walielekea kulia na Esbern alielekea kushoto.
Karibia dunia nzima ilipata habari hiyo na mazungumzo hayo yaliporushwa katika mitandao ya kijamii kila mtu aliliongelea suala hilo kwa namna yake. Wako walitamani Ahata alipize kisasi na wengine wakimuunga mkono. Wengi walitoa maoni yao wakisema kuwa amepumbazwa na uzuri wa Aisha, wengine wanasema kuwa Simba amemloga Ahata akawa ameduwaa tu. Mwaka huo huo Umoja wa Mataifa uliwapatia Ahata na Esbern tunzo ya Amani baada ya masuluhisho yale.
Siku zote hatua tano unazotaka kuzipiga mbele hujui k**a zitakamilika. Usijeukajificha ukasema hakuna aliyekuona bali Mungu anakuona na atatumia namna yoyote siku moja uje uonekane tu. Kulipiza kisasi siyo kwamba ndiyo kumaliza chuki bali ni hatua ya kuendeleza chuki.
TAMATI

Habari ndugu msomaji wa hadithi za Saidikaitastories.com Napenda kukukaribisha katika tamthiliya iitwayo MAPENZI KABURIN...
31/05/2020

Habari ndugu msomaji wa hadithi za Saidikaitastories.com
Napenda kukukaribisha katika tamthiliya iitwayo MAPENZI KABURINI. Ni tamthiliya yenye maonesho matano tu. Ndani yake yamejaa mafunzo mengi sana kwa jamii ya sasa. Karibu sana. Maoni yako ni muhimu sana kwangu.

Pia, tamthiliya hii na hadithi zangu nyingine zitakuwa zinapatikana kupitia blog yangu iitwayo Saidikaitastories

Ahsante.

JINA LA TAMTHILIYA: MAPENZI KABURINIJINA LA MWANDISHI: SAID KAITAMAWASILIANO: 0783372139E-MAIL: Saidikaita7@gmail.comFac...
31/05/2020

JINA LA TAMTHILIYA: MAPENZI KABURINI

JINA LA MWANDISHI: SAID KAITA

MAWASILIANO: 0783372139

E-MAIL: [email protected]

page: Saidikaitastories.com

Blog: Saidikaitastories

ONESHO LA TANO
(Mandhari ya nje ya soko la kilombero. Durudu amevaa boshori, shati la mikono mirefu na suruali nyeusi ya jinsi. Ameweka matunda yake kwenye meza iliyoegeshwa tu miti. Matuda yakiwa ni mapapai, matikiti, mananasi, na maembe na matunda mengi mengineyo. Anaongea na mteja ambaye ni wa jinsia ya k**e. Mteja amevaa dera na kujifunga kishekhati. Durudu anamwambia hivi)
Durudu: Karibu dada matunda bei rahisi tu
ni k**a bure kabisa rafiki jina
nani vile?. Kwasababu huwa
unakuja hapa ila sijawahi
kukuuliza jina lako wakati wewe
ni mteja wangu sana.
Mteja: “ anamjibu huku akitabasamu”
Wewe niite mteja tu.
Durudu: Haya bana mteja. “anatabasamu”
Mteja: Kweli mimi mteja wako. Kwahiyo
niite tu hivyo.
Durudu: Ahaaa Mteja wangu unataka nini
na nini mteja nikufungue?
Mteja: Leo nataka maembe ya elfu
mbili, matikiti mawili, matango
manne, na nanasi moja.
Durudu: Vipi nikuwekee maembe ya juice
au ya nini?
Mteja: Hapana. Fanya mchanganyiko tu
ila sitaki yaliyoiva sana.
Durudu: Ahaa sawa. Hapo sawa. “ anachagua matunda
aliyoelekezwa na kumfungia
kwenye mfuko mweusi. mteja
anampatia fedha ya matunda yale
na Durudu anamrudishia chenji
na mteja wake anasema hivi”.
Mteja: Asante sana.
Durudu: Na mimi nikushuru sana kwa
kuniungisha mzigo wote huu.
Karibu sana. Kweli
Mtejani ni Mfalme.
Mteja: Ahsante… “ huku akitabasamu”
Kwaheri.
“ Mteja anaondoka huku Durudu akiwa anaongea pekee yake kimoyomoyo akisema hivi”. Afadhali huyu mtoto leo hata katia Baraka tena hapa. Kwa sababu hii ni k**a awamu ya tatu anakuja hapa. Ila mteja mzuri kwelikweli. K**a vile ananivutia.sss
“ Mandhari ni ya nyumbani wanapoishi Durudu na huyo jamaa yake ambaye anaitwa Kijukuu. Wamepangisha chumba kimoja huko majengo. Wamekaa nje na maongezi kidogo yakiwa yamewatawala. Huyo kijukuu kavaa kisuruali kimembana kwelikweli na boshori lake la rangi ya bluu na kavalia na sweta juu. Durudu naye amevaa jinsi na tisheti nyeusi. Jua limewaka ni kivulini wamekaa ”.
Kijukuu: Oya chalii yangu eeee naona
k**a vile unapaogopa ogopa sana
hapa mageto. Sijui k**a vile
hujapazoea au vipi?
Durudu: Kwanini Kijukuu?
Kijukuu: Naona unaishia na mademu huko
mbali tu. K**a unataka kupiga
demu kuwa huru wewe
unaniambia tu tayari mimi
nakuachia nanja najua kabisa
chalii anapiga kitu.
Durudu: Haina shida unajua kuku mgeni hakosi kamba mguuni. Kwahiyo
wala usihofu.
Kijukuu: Hamna imenibidi tu nikuambie
mapema ili usije ukaanza
kuogopa na kuanza
kuwapeleka mademu huko guest
na unamaliza hela bure wakati
geto la muhuni ambalo kwasasa
ni la wahuni liko hapa.
Durudu: Hamna noma.
Kijukuu: Kwahiyo embu hiyo kamba
iondoe mguuni mapema sana.
Hapa mjini usikae kiwakiwaki tu
chalii yangu. Watoto wazuri
wanakuja kila siku kununua
matunda halafu unabaki kuumia
tu wakati uwezekano upo kabisa.
Wewe ukiona tu vipi
umeshajinyakulia huko tayari
wewe nijulishe tu ili nisije
nikaingilia mechi yako hapa.
Durudu: Hamna noma.
Kijukuu: Siku za jumapili ndiyo huwa hapa hawa wapangaji wenzangu huwa
wanakuweko sana hapa
nyumbani ila ndiyo hivyo ukileta
demu wako unawawekea
wambuzi tu. Hakuna kucheka
na kima hapa. Una demu wako
umewakuta hapa ni salamu ndani inatosha.
Durudu: Hapo nimekupata Kijukuu.
Kijukuu: Hamna noma bablai mbona
wananimanya sana
hapa.Wanamjua kabisa
Kijukuu ni nani.
“ Ni mazingira ya ndani wanapoishi Kijukuu na Durudu. Durudu anaonekana yuko na msichana aitwae Mwatabu. Wako kitandani wamejifunika shuka hapo wanaonekana wameshamaliza shughuli. Mwatabu kwa sura tu amejaaliwa, mdomo uliokaa vizuri kwa ajili ya kazi maalum ya tukio lililotokea kwa muda si mrefu kati ya Durudu na Mwatabu”.
Durudu: Sasa Mwatabu tutakuwa
tunatumia kondomu hadi lini
hivi?
Mwatabu: Hadi tukapime kwanza ndiyo
hapo nitaprove.
Durudu: Unajua ni k**a haina ladha
kabisa.
Mwatabu: Wewe ndiyo unafanya isiwe
na ladha kabisa.
Durudu: Kwanini?
Mwatabu: Kwani tungepima tukajua afya
zetu mbona hata hiyo ladha
ungeipata vizuri tu.
Durudu: Ila Mwatabu kwa kweli wewe
tambua tu mimi sina malengo ya
kukuchezea tu mimi nataka
nikuoe kabisa.
Mwatabu: Mimi mwenyewe na malengo na
wewe kwamba niolewe na wewe. Wewe ukafikiri mimi siyatamani mambo uliyonipa hapa muda si
mrefu? Nayatamani sana Ila
k**a ndiyo hivyo hutaki kupima tutaishije hapo? Mimi siwezi
kuishi na mwanaume ambaye
sijapima nae kabisa hivi
nikahakikisha. Kwasasa Durudu
kuna magonjwa mengi tu, kuna
huu UKIMWI ambao watu
wanaondoka k**a vile vivuli
bila hata kujijua. Kweli mimi
niko tayari kuolewa na wewe ila
k**a tu ukikubali tukapime.
Durudu: Haya haina shida. Tulia
nitakujulisha.
Mwatabu: Mimi tayari muda wowote tu.
Durudu: Haya. “ wanainuka pale na kila
mtu anavaa nguo na tayari
wanatoka nje na wanaagana
tayari Mwatabu anaondoka na
kumuacha Durudu akiwa
amesimama tu k**a msitimu
usiounganishwa nyaya.kisha
Durudu akawa anaongea pekee
yake akisema hivi” Yaani hawa
watoto wa mjini sijui wakoje.
Huyu Mwatabu sijui amejua
mimi nina UKIMWI ndiyo maana
ameng’ang’ania kwelikweli.
Huyu mjinga kweli, mimi cha
msingi nimeshamlamba basi
apite hivi. Wangapi hapa mtaani
nimewalamba kavu tu. Kwanza
tangu nizaliwe leo ndiyo
nimetumia kondomu. Yaani
utafikiri msumeno siwezi
kufanya upumbavu huu.
Ingekuwa kisu kinachinja na
hala yake hapo sawa. Sifanyi huo
ujinga. Nimeshawapitia wengi tu
kavu na nitaendelea kuwapita
kavu. Ila mtamu
kwelikweli k**a sura yake ilivyo.

“ Ni muda wa miaka miwili na miezi kadhaa. Durudu ameshaanza kuishi pekee yake. Biashara zinaenda vizuri sana. Alipopangisha ni sehemu yenye vyumba viwili maeneo ya hapo hapo majengo ya chini. Lakini muda huo anaonekana yuko chumbani kwake na msichana hapo wakiwa tayari wameshapeana utamu. Kitandani wakiwa wamejifunika shuka. Durudu anamwambia huyo mwanadada hivi”
Durudu: Daaaa unajua Doli wewe mtamu
sana. Daaa kweli Mungu
amekujaalia kabisa.
Doli: Wala mbona kawaida tu.
Durudu: Kweli. Daaa kweli Tanga
mmejaaliwa na ndiyo maana
wakasema ndiko yalikozaliwa
huko. Siwezi kupinga kwa
nilichokiona leo.
Doli: Wewe nisifie tu halafu uje
kuniacha hapa. Kwa sababu nyiye wanaume bana sijui mkoje?
Durudu: Hapana Doli mimi siwezi
kukuacha kabisa. Mimi na wewe
namuomba Mungu tudumu
milele. Mimi matarajio yangu ni
kukuoa kabisa.
Doli: Haya mimi niko tayari.
Durudu: Unajua Doli kwasasa
nimeshakuwa umri unaenda.
Nikisema nimrukie mwanamke
huyu kesho Yule sasa kweli
mwisho wa siku hata Mungu
atanilaani nikajikuta nahangaika
tu na hao wasichana tu badala ya kutafuta maisha. Yaani mimi leo
hii ingekuwa nahangaika tu na
hao wasichana leo hii
nisingekuwa naishi kwenye hiki
chumba pekee yangu. Sasa hivi ni
mwaka wa pili hivi nahisi
unakaribia kukata kabisa
nimekuja hapa nikiwa nakaa
mageto kwa rafiki yangu tu.
Kwahiyo kwasasa ni muda wa
mimi kuweza kupata mwenza wa
kuniburudisha na hadi tuoane
kabisa. Doli nina malengo na
wewe embu niamini.
Doli: Sawa nitakuamini k**a na wewe
utakuwa kweli na hayo malengo.
Durudu: Sawa. Ila unajua Doli kuna jambo
nataka nikujulishe sijui
utalipokeaje!
Doli: Niambie ndipo nijue nitalipokeaje.
Durudu: Yaani hadi naogopa kukwambia.
Doli: Niambie na mimi nijue nitaogopa
au laaa.
Durudu: Aaaaaaa Doli kwamba….
Unajua… Doli…
Doli: Mbona kigugumizi cha ghafla tu?
Kimetokea wapi? Embu ongea bana.
Wewe hujui mimi hapa mimi ni
mfanyakazi wa ndani nanimetoroka tu kwa vile nimeaga naenda
kusalimia marafiki zangu. Embu
niambie bana Durudu mimi
niwahi zangu.
Durudu: Isiwe tabu sana. Aaaa… Doli mimi
… nime… nimeathi…athirika.
Doli: “ haamini alichokisikia kutoka
kwa Durudu. Doli anasema”.
Durudu ati unasemaje?
Durudu: Nina UKIMWI.
Doli: UKIMWI… UKIMWI kabisa huu
ninaoujua. Yaani kabisa Durudu
umeamua kunichinjia baharini
kabisa. Durudu sasa mimi
nitamueleza nani haya majanga
kabisa. Durudu mimi Yule bosi
wangu hatanielewa kabisa. Hivi
eeeee Mungu wangu weeee kweli
kuna watu hampendi kabisa
maendeleo ya wenzenu. Ooooooh!!! jamani kuna watu ni chui. Durudu
kabisa na hatujatumia hata cha
kondomu.
Durudu: Doli usikasirike ndiyo
imeshatokea hivi.
Doli: Imetokea hivi… yaani unaongea
kirahisi kabisa. “ anaongea huku
machozi yakimbubujika
kwelikweli”
Durudu:Ndiyo maana nimeahidi nitakuoa
Doli siwezi kukuacha k**a
ukikubaliana na mimi. Hiyo ndiyo
imeshatokea tayari.
“ Doli anainuka kwa hasira anavaa nguo na pia Durudu naye anainuka na kuanza kuvaa nguo haraka haraka ili amsindikize Doli. Anampa maneno ya kumtia moyo. Wanatoka nje wanatembea wote hadi sehemu yenye boda boda na wanapakia kwenye piki piki moja. Doli anapoishi ni huko kwa Morombo”.

“ Mandhari ya nyumbani kabisa kwa Durudu. Ambapo Durudu alijitahidi hadi kufikia kujenga nyumba yake kabisa yenye vyumba vinne hapo ni baada ya k**a ya miaka mitano kabisa. Wanaonekana wamekaa Doli na Durudu wakiwa wana maongezi ya hapa na pale. Doli amevaa dera na kichwani kajifunga kitambaa chekundu huku Durudu akiwa amevaa suruali ya kitambaa na shati jeupe.walipokaa ni kwenye makochi. Nyumba yake kwa huko juu bado haijakamilika vizuri yaani haina silingiboard. Wanaangalia runinga”.
Durudu: Doli mke wangu. Kwasasa ni muda tayari umeshapita tangu tuingie
kwenye ndoa yetu. Majanga mengi
tumeyapata hadi muda huu na
moja wapo ni hilo la wewe
kuharibika kwa mimba yako.
Niseme tu nikushukuru kwa
uvumilivu wako.
Doli: Sawa.
Durudu: Pia ndiyo hivyo hata sasa afya
yako si nzuri sana. Ila bado nasema nitaendelea kuwa na wewe. Kwa
sababu haya yote ni mimi k**a
msababishaji ila kwasasa si muda
wa kuanza tena kulaumiana au
kulalamika bali ni muda wa sisi
kujipanga ipasavyo tujue ni namna
gani ya kujiendeleza zaidi ya
tulipofikia muda huu.
Doli: Sawa mume wangu nimekuelewa.
Durudu: Aaaah ni kwamba unakumbuka
kuhusu mwanangu na mdogo
wangu wako nyumbani kule
niliwaacha.
Doli: Ndiyo uliniambia vipi kwani kuna
nini huko?
Durudu: Aaaaah… hamna ila nilitaka tu
nikujulishe kwamba nataka
nikawachukue niwalete huku
mjini wafanye kazi nao na Yule
mwanangu aje aendelee na
masomo huku. Kwasababu
kwasasa Yule Ilali ambaye ndiyo
mdogo wangu ameshakuwa ni mtu
mkubwa kabisa hata ukimwambia
simamia sehemu fulani anaweza
kufanya hivyo kabisa.
Doli: Haina shida itakuwa ni vyema
ukifanya hivyo. Kwasababu ndiyo
hivyo hata afya yangu ndiyo k**a
unavyojionea hapa. Hiyo kansa ya
koo niliyonayo hapa hii ni muda
wowote tu natumai itanichukua.
Ukichanganya na huo UKIMWI
ndiyo kwaheri kabisa.
Durudu: Embu bana usiongelee kuhusu hilo
jambo kabisa.
Doli: Ndiyo ukweli huo. Ila sawa.

“ Ni nyumbani kwa Durudu tunaona Doli akiwa amelala kitandani. Durudu akiwa amesimama hapo pamoja na Ilali na Ijojo. Doli anaonekana hali yake si nzuri kabisa sauti anayoitoa ni sauti ya chini sana. Anaongea k**a vile sauti inakata kata. Ilali anaonekana kabisa ameshakuwa ni mrefu kabisa na hata Ijojo naye ameshakuwa kabisa si k**a wa kipindi kile. Muda huo ni mishale ya saa kumi alasiri. Durudu anamuongelesha Doli”
Durudu: Mke wangu unajisikiaje?
Doli: “ Anaongea kwa shida lakini hata
hasikiki kabisa. Anaongea kwa
ishara akiwa anauonyooshea
mkono wake shingoni”.
Durudu: Sasa Ilali embu angalia kwenye
simu yangu hapo angalia kuna
namba imeandikwa Tax embu
mpigie halafu mwambie aje hapa
nyumbani kwangu muda huu.
Ilali: Sawa kaka. “ Ilali anaenda
kuchukua simu ikiwa kwenye
kochi. Simu ni aina ya TECNO
ndogo tu. Anaingia kwenye orodha
ya majina na kutafuta TAX anapiga
simu”.
Durudu: Embu Ijojo chukua baadhi ya
nguo za mama yako na uweke
kwenye mkoba ili TAX ikija tu
isiwe shida tena.
Ijojo: Sawa baba.
Durudu: Sasa Ijojo itabidi ubaki hapa
nyumbani kwa ulinzi zaidi. Sisi
tutaenda hospitali pamoja na Ilali.
Ijojo: Sawa baba.
“TAX inasikika huko nje ikiwa inaliza honi. Tayari Doli anainuliwa. Durudu, Ilali, na Dereva ndiyo wamembeba na kumpeleka kwenye gari. Wote wanaingia ndani ya gari na dereva anakanyaga gia kueleka MOUNT MERU HOSPITAL”.

“ Inaonekana ndiyo panapambazuka. Daktari pamoja na rafiki wa Doli ambaye ndiye aliyekuwa amelala na Doli wodini wana maongezi huku wakiwa wanatembea. Wanakutana na Durudu akiwa ameshikilia kikapu chenye chupa na vitu vingine vikiwa vimefunikwa. Daktari anakatisha mazungumzo baada ya kumuona Durudu na pia rafiki yake Doli naye anaonekana yuko kimya Durudu anasema”.

Durudu: “ Akiongea akiwa na hamasa ya
kujua hali ya Doli” Dokta vipi hali
ya mke wangu?
Daktari: Aaaaah …. Kuwa huru kwanza za
nyumbani?. Uko swalama kabisa?.
Shemeji: “ anaonekana anampokea
Durudu kikapu.”
Durudu: Huko hawajambo kabisa. “ Ilali
pia naye anaonekana anakuja
anawakuta wakiwa katika
mazungumzo” vipi mke wangu?
Daktari: Aaaaa?…. Durudu hali ya Mama
si nzuri sana….
Durudu: Si nzuri ni sawa tangu jana hali si
nzuri embu nielezenivizuri.i
Daktari: Aaaa… kwa ujumla… ame…
amefariki alfajiri…
Durudu: “ Baada ya kuambiwa tu anabaki
ameduwaa tu hana hata la
kuongea. Daktari anamwambia
hivi.”
Daktari: Unajua mipango ya Mungu haina
makosa.
Durudu: Naruhusiwa kwenda kumuangalia
muda huu.
Daktari: Embu tulia kwanza kwasasa hivi
embu tuende kwanza sehemu ya
Mapumziko. Kwasababu tayari
tumeshampeleka mwochari…
kwahiyo embu ungetulia kwanza.

“ Ni siku ya nne baada ya maziko kufanyika. Mandhari inayoonekana ni nyumbani kwa Durudu panaonekana watu wakiwa wamekaa makundi makundi wakiwa na mazungumzo ya hapa na pale. Ilali na Ijojo wakiwa nao wako kibarazani hapo, baadhi ya ndugu wa Durudu wako pale katika kikao hicho kilichokuwa kinahusu ugawaji wa mirathi. Muda huo ilikuwa ni mishale ya saa nne asubuhi. Panaonekana kuna meza pia juu ya meza kuna matunda yamewekwa ili watu wajipatie kula. Pia kuna kisu cha kukatia matunda kipo hapo kinaonekana. Shemeji zake Durudu nao wako hapo na binamu zake pia wako hapo pamoja na Kijukuu katika kikao hicho. Durudu anasema hivi”.
Durudu: Habarini ndugu, jamaa na
marafiki.
Wote: Salama.
Durudu: Mkusanyiko huu unamaanisha
kuna mazungumzo maalum.
Baadhi ya watu natumai
hawakuwa wanawajua wadogo
zangu na mwanangu. Huyu hapa
ni Ijojo (Ananyoosha kidole kwa
Ijojo ) ndiyo mwanangu wa kwanza na huyu hapa (Ananyoosha kidole
kwa Ilali) ni Ilali ni mdogo wangu
na katika familia yetu tumezaliwa
wawili tu yaani mimi na huyu Ilali.
Pia ndiyo huwa naishi nao wote
hawa hapa nyumbani. Pia tangu
mwanzoni tu hawa ndiyo k**a
warithi wa vitu mbalimbali
ambavyo ni vyangu. K**a nyumba hii tayari ilikuwa imeshaandikwa
hii ni yao yaani kwa wote.
Nimependa kusema tu hivi
kwasababu hakuna ajuae badae
wala kesho. Nyumbani kule nako
panajulikana baadhi ya maeneo
ambayo ni ya kwao ya ushikirika
yaani kati ya Ilali na Ijojo.
Embu Ilali na Ijojo wasalimuni
ndugu zenu hapa.
Ilali: (Anasimama ili kutaka kuwasalimia ndugu. Durudu anaonekana
anachukua tunda hapo mezani.
Anachukua na kisu, analikata
chungwa huku akiwa anawaza
sana ni watu wengi ameshawaua
sana kwa huo ugonjwa wa UKIMWI.
Anamfikiria aliyempa UKIMWI
ambaye ni Safi, baadhi ya wasichana wake wote aliyowapitia na
kuwapatia UKIMWI hadi
anamkumbuka mke wake ni yeye
ndiye kamuambukiza UKIMWI na
kafariki. Pale pale anaamua
kujichoma kisu kifuani na
anaanguka chini watu wanashangaa
tu mtu yuko chini. Wanaanza
kumnyenyua ili kumpeleka hospitali
tayari anafariki hapo hapo).

TAMATI

Address

Dar Es Salaam

Alerts

Be the first to know and let us send you an email when Mwandishi Said Kaita posts news and promotions. Your email address will not be used for any other purpose, and you can unsubscribe at any time.

Share

Category